TCB YAWEKA MKAKATI KUKUZA SOKO LA KAHAWA NCHINI

MOSHI-KILIMANJARO.

BODI ya Kahawa Tanzania (TCB), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa zao hilo, imeweka mkakati wa kuongeza matumizi ya kahawa nchini kutoka asilimia saba ya sasa hadi kufikia asilimia 15, hatua inayolenga kukuza soko la ndani na kuongeza mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa.

Mkurugenzi wa Masoko wa TCB, Frank Nyarusi, alisema hayo mjini Moshi, wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika uzinduzi wa Msimu wa Saba wa Kahawa Festival, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bodi hiyo.

Nyarusi alisema TCB kwa kushirikiana na wadau wote waliopo katika mnyororo wa thamani wa kahawa, imetenga mwezi mzima kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa zao hilo, ikiwemo kuongeza uelewa, ubunifu, uzalishaji, ubora na matumizi ya kahawa ndani ya nchi.

Alisema kahawa ni zao lenye fursa nyingi za kibunifu na kiuchumi, hivyo ni muhimu kwa wadau kuendelea kubuni bidhaa na huduma mbalimbali zinazotokana na kahawa, sambamba na kuhamasisha matumizi yake nchini.

“Zao la kahawa ni zao bunifu, kila wakati kuna jambo jipya la kibunifu linaloweza kufanyika katika jamii, lengo letu ni kuongeza uelewa kuhusu zao la kahawa na kuongeza unywaji wa kahawa,” alisema Nyarusi.

Alisema kwa sasa ni asilimia saba pekee ya Watanzania wanaotumia kahawa, huku asilimia 93 ya kahawa inayozalishwa nchini ikiuzwa katika masoko ya nje ikiwa katika mfumo wa clean coffee.

Kaulimbiu ya Msimu wa Saba wa Kahawa Festival inasema: “Kahawa Ni Sehemu ya Suluhisho , Kujenga Ustawi Kupitia Mashindano,” ikiwa inalenga kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili zao hilo na kutumia fursa zilizopo kulikuza zaidi.

Nyarusi alisema mkakati wa TCB na wadau wake ni kuongeza matumizi ya kahawa ndani ya nchi kutoka asilimia saba hadi kufikia asilimia 15, hatua ambayo itasaidia kukuza soko la ndani na kuongeza thamani ya zao hilo.

Aidha, alisema uzalishaji wa kahawa nchini umeendelea kuongezeka, kutoka wastani wa tani 50,000 kwa miaka ya nyuma hadi kati ya tani 80,000 na tani 100,000 kwa sasa.

Alisema katika msimu wa 2025/26, sekta hiyo ilivunja rekodi baada ya mauzo ya kahawa kufanikisha zaidi ya Sh trilioni moja kuingia kwa wakulima, jambo alilosema linaonyesha umuhimu wa zao hilo katika kuongeza kipato kwa wananchi na kuchangia uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kahawa Festival, Denis Mahulu, alisema TCB imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa miche ya kahawa kutoka miche 20,000 iliyozalishwa katika msimu uliopita hadi miche 30,000 katika msimu wa 2026/27.

Alisema hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya miti ya kahawa na hatimaye kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini, huku lengo la muda mrefu likiwa kufikia uzalishaji wa tani 300,000.

Mahulu alisema kupitia Kahawa Festival, wadau wa sekta hiyo wanapata fursa ya kukutana, kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili mnyororo wa thamani wa kahawa, kuanzia uzalishaji, uchakataji, uongezaji thamani hadi masoko.

Kuhusu masoko, alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza ubora wa kahawa ya Tanzania, kutafuta fursa mpya za masoko na kuimarisha yaliyopo.

Alisema maonesho hayo pia yanalenga kukuza soko la ndani kwa kuongeza matumizi ya kahawa, pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuanzisha bidhaa na biashara mpya zinazohusiana na kahawa Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizindua Msimu wa Saba wa Kahawa Festival, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema ili kuongeza ushindani wa kahawa ya Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa, ni muhimu kwa wadau kuendelea kuzingatia ubora, uendelevu na viwango vinavyohitajika katika masoko mbalimbali.

Mnzava pia aliwataka wadau wa sekta hiyo kutumia teknolojia za kidijitali na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano na biashara katika kuitangaza chapa ya kahawa ya Tanzania, kutafuta masoko mapya na kuimarisha masoko yaliyopo.

Alisema matumizi ya teknolojia yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuwafikia walaji na wanunuzi wa kahawa ndani na nje ya nchi, hivyo kuongeza ushindani na thamani ya zao hilo katika soko la kimataifa.

Aliongeza kuwa "Mkakati huo unalenga kuifanya kahawa kuwa zao lenye manufaa zaidi kwa mkulima, mfanyabiashara na taifa kwa kuongeza uzalishaji, matumizi ya ndani, thamani ya bidhaa na fursa za masoko.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.