MOSHI-KILIMANJARO.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imetenga maeneo maalumu katika vituo vya afya kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi endapo kutatokea milipuko ya magonjwa inayoweza kujitokeza kutokana na mvua za Vuli zinazotarajiwa kuanza kunyesha Oktoba mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, aliyasema hayo jana wakati wa katika kikao kazi kati yake na watendaji wa ngazi ya kata na mitaa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo.
Nasombe alisema kuwa mvua hizo zinaweza kuambatana na changamoto mbalimbali, ikiwemo uwezekano wa kutokea kwa milipuko ya magonjwa, hivyo Manispaa imeanza kuchukua hatua za tahadhari ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati endapo changamoto hiyo itajitokeza.
"Manispaa kupitia Kamati zetu za ndani tumejiandaa kwa kutenga maeneo maalumu, likiwemo eneo katika Kituo cha Afya Msandaka, ambalo litatumika kuhudumia wananchi watakaopata magonjwa ya milipuko."alisema Nasombe.
Aliongeza kuwa “Ziko athari ambazo tunaweza kuzipata wakati wa mvua hizi za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha, ikiwemo milipuko ya magonjwa. Sisi kama Manispaa tumejiandaa kupitia kamati zetu za ndani na tumetenga maeneo maalumu, endapo itatokea changamoto hiyo, watu watakaopata magonjwa ya milipuko watapelekwa katika Kituo cha Afya Msandaka,” alisema.
Nasombe aliwataka watendaji wa kata kuhakikisha wanafahamu maeneo yaliyotengwa na Manispaa ili endapo kutatokea mlipuko wa magonjwa, wananchi walioathirika waweze kuelekezwa na kupelekwa katika maeneo hayo kwa ajili ya kupata matibabu na huduma nyingine zinazohitajika.
Aidha, aliwataka watendaji wa kata na mitaa kusimamia usafi wa mazingira, hususan kuhakikisha mifereji ya kupitisha maji ya mvua inakuwa safi na inapitisha maji kwa ufanisi, ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa na mafuriko.
Nasombe alisisitiza kuwa usafi na utunzaji wa mifereji ni muhimu katika kuzuia maji kuziba njia, mafuriko na uharibifu wa miundombinu, huku akiwataka watendaji kuhakikisha maandalizi yanafanyika mapema kabla ya mvua hizo kuanza.
Diwani wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, alisema tayari wameanza kuchukua hatua za kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo kwa kusafisha mitaro na kuondoa tope pamoja na udongo uliotuama katika mifereji inayopitisha maji ya mvua katika kata hiyo.
Shekoloa alisema zoezi hilo linafanyika kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo, akieleza kuwa ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha mifereji inakuwa katika hali nzuri na inapitisha maji kwa ufanisi wakati wa mvua, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko na uharibifu wa miundombinu.




