MOSHI-KILIMANJARO .
WANANCHI wanaoishi katika maeneo ya mabondeni, milimani, yenye miteremko mikali pamoja na maeneo yenye mifumo duni ya kupitisha maji, wametakiwa kuchukua tahadhari zaidi kuelekea msimu wa mvua unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu, kufuatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Abraham Urio, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu utabiri wa mvua hizo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na wananchi ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.
Urio alisema wananchi wanaoishi katika maeneo ya milimani, mabondeni, kwenye miteremko pamoja na maeneo yenye mifumo duni ya kupitisha maji wanapaswa kuwa makini zaidi, kwani mvua kubwa zinaweza kusababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi na uharibifu wa miundombinu pamoja na mali
Aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na TMA na kuchukua hatua mapema pale wanapoelekezwa kufanya hivyo, ikiwemo kuondoka katika maeneo hatarishi na kwenda sehemu salama, ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi
Aidha, Urio alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kutunza mazingira, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza athari za mvua kubwa na mafuriko.
"Wananchi wanapaswa kuepuka shughuli zinazoweza kuharibu mazingira, hususan katika maeneo ya milimani, mabondeni na maeneo yanayohifadhi vyanzo vya maji."alisema Urio
Historia inaonyesha kuwa msimu wa mvua wa mwaka 1997/1998 ni miongoni mwa misimu iliyoshuhudia kiwango kikubwa cha mvua nchini Tanzania, hali iliyosababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali na kuleta uharibifu wa miundombinu na mali.
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limewahi kuhusisha mvua hizo na athari za hali ya hewa ya El Nino.
Zaidi ya miongo miwili baadaye, Tanzania ilikumbwa tena na mvua kubwa zilizohusishwa na El Nino katika Msimu wa 2023/2024, ambazo zilisababisha madhara katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo maporomoko ya ardhi katika Mlima Hanang, mkoani Manyara, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 80.
Pia, Novemba 2009, watu 24 walipoteza maisha katika eneo la Manka, Kata ya Mamba Myamba, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, baada ya kutokea kwa maporomoko ya udongo yaliyohusishwa na mvua kubwa zilizonyesha mfululizo kwa siku kadhaaa, tukio hilo lilisababisha pia uharibifu mkubwa wa makazi na mali za wananchi.
Kutokana na historia hiyo, wananchi wameendelea kusisitizwa kuchukua tahadhari mapema, kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia maelekezo ya mamlaka husika, hususan katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi.







