BARAZA LA HALMASHAURI WILAYA YA SIHA LIMEWAFUKUZA KAZI WATUMISHI WAWILI, WANNE WAPELEKWA KITUO CHA URAIBU

SIHA-KILIMANJARO. 

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, limewafukuza kazi watumishi wawili kwa utoro kazini, huku watumishi wengine wanne wakipelekwa katika kituo maalumu cha huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya, baada ya kubainika kuwa wanatumia pombe kupita kiasi hali iliyoathiri utekelezaji wa majukumu yao.

Akisoma uamuzi wa Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Dancan Urassa, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya baraza kupitia mashauri ya kinidhamu dhidi ya watumishi hao na kubaini kuwa walikiuka sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Amesema watumishi waliofukuzwa kazi ni Muuguzi Daraja la Kwanza wa Hospitali ya Wilaya ya Siha, Vitalis Christopher Bajuta, ambaye alibainika kuwa na utoro wa siku 104, pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Lawate, Joel Steve Mulenga, aliyebainika kutoroka kazini kwa siku 156.

Amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 42 ya utumishi wa umma, mtumishi anayefanya utoro kazini kwa siku tano au zaidi anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu, na kwamba baada ya taratibu zote kufuatwa, Baraza limeridhia watumishi hao wawili kufukuzwa kazi.

Amesema halmashauri haitasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaokiuka wajibu wao, ikiwemo utoro, ulevi na ubadhirifu wa mali za umma, huku akiwataka watumishi kuzingatia sheria na taratibu za utumishi ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Hellen Mwambeta, amesema kabla ya kufikia uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi hao, halmashauri ilichukua hatua mbalimbali za kinidhamu, ikiwemo kuwaita kwenye vikao, kuwaelekeza na kuwashauri, lakini utoro uliendelea.

Mwambeta amesema watumishi wanne waliobainika kutumia pombe kupita kiasi wamepelekwa katika kituo maalumu cha uraibu kwa kipindi cha miezi mitatu, ambapo gharama za matibabu na huduma wanazopata zinagharamiwa kwa pamoja na halmashauri pamoja na wazazi wao

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha wamesema hatua hizo za kinidhamu ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma, huku wakisisitiza kuwa watumishi wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ajira ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.