MOSHI-KILIMANJARO.
WAZIRI wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa, anatarajiwa kuongoza washiriki zaidi ya 3,000 katika mbio za Lung Health Half Marathon, zinazotarajiwa kufanyika Novemba 8, mwaka huu katika Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI), Wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake, ambapo amesema mbio hizo zinalenga kuchangisha Sh bilioni 3 kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu na uangalizi wa muda mrefu, hususan wenye magonjwa sugu na matatizo ya afya ya mapafu.
Alisema fedha zitakazopatikana zitatumika katika ujenzi na uwekaji wa vifaa tiba, katika wodi maalumu, kuimarisha huduma ya oksijeni, uchunguzi na uhamasishaji kuhusu afya ya mapafu, pamoja na kusaidia utafiti na huduma nyingine zinazolenga kuboresha afya ya mfumo wa upumuaji.
“Kipaumbele kitakuwa kwa wagonjwa walioathiriwa na vumbi la kikazi (Silicosis na TB) hususani katika mazingira yenye shughuli za uchimbaji madini na shughuli nyingine zinazoweza kuongeza athari za magonjwa ya mapafu, pamoja na wananchi kutoka jamii zinazozunguka wanaohitaji huduma maalumu za afya ya mapafu,” alisema.
Alisema mbio hizo si tukio la michezo pekee, bali ni tukio linalounganisha afya, michezo, jamii, kumbukumbu, utalii na uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya, huku zikiwa pia sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 ya TIDI, ambayo kilele chake kinatarajiwa kufanyika Novemba 11, mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAAA), Nelson Mrasha, alisema chama hicho kina jukumu la kusimamia mbio za riadha mkoani humo kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Tanzania (R T) pamoja na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), ambao wana dhamana ya kutoa vibali vya mashindano hayo.
"Mbio hizi zitashirikisha wakimbiaji zaidi ya 3,000 katika umbali wa kilomita 21, kilomita 10, kilomita 5, pamoja na mbio za watoto za kilomita 2.5, huku akiwataka wadau mbalimbali kujitokeza kushiriki na kutoa mchango wao ili kufanikisha lengo la tukio hilo."alisema.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, amepongeza uongozi wa TIDI kwa kuja na wazo la kuandaa mbio hizo, akisema tukio hilo litasaidia pia kuitangaza taasisi hiyo, hususani baada ya kupandishwa hadhi na kuwa taasisi kamili.
Aidha alisema Tanzania imeendelea kuwa eneo linaloweza kutoa huduma bora za matibabu kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya afya, vifaa tiba na uwepo wa wataalamu waliobobea.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TIDI, Dk. Leonard Subi, alisema moja ya malengo ya mbio hizo ni kuhakikisha wanapata rasilimali za kujenga wodi maalumu itakayokuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya wagonjwa wa Silicosis na TB, ambao wanaohitaji huduma na uangalizi wa muda mrefu.
“Tumejipanga vizuri kwa ajili ya watu kukimbia, lakini pia tunataka watu wahamasike kutunza afya zao na miili yao kupitia michezo,” alisema Dk. Subi.
![]() |


















