KILI PLANTATION YATINGA NUSU FAINALI ZUBERI CUP

MOSHI-KILIMANJARO.

TIMU ya Kili Plantation FC imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Zuberi Cup baada ya kuiondoa Kibo Warriors FC kwa mikwaju ya penalti 5-3, kufuatia sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida wa mchezo.

Katika mchezo huo uliochezwa majira ya saa 10 jioni, Kili Plantation FC ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya tano kupitia kwa Noel Mbuya, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti na kuiweka timu yake mbele.

Kibo Warriors FC ilirejea kipindi cha pili ikiwa na dhamira ya kusawazisha na dakika ya 47, Makambo Yange aliifungia timu hiyo bao la kusawazisha, Kili Plantation FC haikukata tamaa na dakika ya 71, Daudi Mtui aliifungia timu yake bao la pili na kuifanya Kili Plantation FC kuongoza kwa mabao 2-1.

Hata hivyo, Kibo Warriors FC iliongeza mashambulizi na dakika ya 76 Makambo Yange alifunga bao lake la pili katika mchezo huo, na kuisawazishia timu yake hadi mchezo ulipomalizika kwa sare ya mabao 2-2, hali iliyolazimu mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penalti.

Katika mikwaju hiyo, Kili Plantation FC ilionyesha umakini zaidi kwa kufunga penalti zote tano, huku Kibo Warriors FC ikifanikiwa kufunga penalti tatu, wakati mkwaju mmoja ukidakwa na kipa wa Kili Plantation FC na kuipa timu hiyo ushindi wa jumla wa 5-3.

Kwa matokeo hayo, Kili Plantation FC imeungana na La Familia FC pamoja na Kilimanjaro Wonders FC katika hatua ya nusu fainali ya Zuberi Cup, huku timu nyingine itakayokamilisha idadi hiyo ikijulikana baada ya mchezo wa kesho, Agosti 14, 2026.

Kesho macho ya mashabiki wa soka yataelekezwa katika Uwanja wa Railway Njoro, Moshi, ambako kutakuwa na mpambano mkali kati ya Fire FC na Hai United, huku kila timu ikisaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.























Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.