SERIKALI YATOA TRIONI 1.57 KUTEKELEZA MIRADI 2,445 YA MAENDELEO KILIMANJARO

MOSHI-KILIMANJARO.


SERIKALI imetoa jumla ya Shilingi trilioni 1.57 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani Kilimanjaro kati ya Machi 2021 na Mei mwaka huu, hatua iliyowezesha kutekelezwa kwa miradi 2,445 katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Abraham Urio, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa waandishi wa habari mjini Moshi.

Urio alisema fedha hizo zimeiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo mbalimbali ya kitaifa, huku zikichochea utekelezaji wa miradi katika sekta za afya, elimu, maji, barabara, kilimo, mifugo, usafirishaji, mipango miji, utalii na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi

Alisema katika sekta ya afya, Serikali imeimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa zaidi ya asilimia 90, sambamba na ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo jengo la tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani na jengo la wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC.

Mafanikio mengine aliyoyataja ni pamoja na ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto, jengo la huduma za dharura na ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, pamoja na ujenzi wa maabara ya kisasa ya afya ya jamii na mtambo wa kuzalisha oksijeni katika Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto.

Kwa mujibu wa Urio, katika kipindi hicho hospitali za wilaya zimeongezeka kutoka mbili hadi nane, vituo vya afya kutoka 28 hadi 48 na zahanati kutoka 198 hadi 258, huku vifo vitokanavyo na uzazi vikishuka kutoka 51 hadi 33 kwa kila vizazi hai 100,000.

Katika sekta ya elimu, alisema Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa elimu bila ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 91.78 zimetumika kati ya mwaka 2020 na 2025. Aidha, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 1,007 hadi 1,049 na shule za sekondari kutoka 281 hadi 317.

Alisema mafanikio hayo yameenda sambamba na kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu pamoja na kuimarika kwa ufaulu wa mitihani ya darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita.

Akizungumzia sekta ya miundombinu, Urio alisema mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 1,239 hadi 1,328, huku barabara za changarawe zikiongezeka kutoka kilomita 878 hadi 1,589. Pia madaraja yameongezeka kutoka 254 hadi 355 na barabara mpya zenye urefu wa kilomita 815 zimefunguliwa.

Alisema Serikali imeboresha upatikanaji wa maji safi ambapo huduma hiyo imefikia asilimia 84.5 vijijini na asilimia 99 mijini, huku mradi mkubwa wa maji wa Same–Mwanga–Korogwe ukiwa umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo.

Katika sekta ya nishati, Urio alisema vijiji vyote 519 vya Mkoa wa Kilimanjaro vimeunganishwa na umeme, huku vitongoji 2,074 kati ya 2,260 vikifikishiwa huduma hiyo. Aidha, Serikali imetenga Shilingi bilioni 33.53 katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji 186 vilivyosalia.

Kwa upande wa kilimo, alisema Serikali imejenga na kukarabati skimu 12 za umwagiliaji, hatua iliyoongeza idadi ya wanufaika wa kilimo cha umwagiliaji kutoka wakulima 11,144 hadi 13,349. Pia upatikanaji wa mbolea ya ruzuku umeongezeka kutoka tani 18,826 hadi tani 75,786, huku wakulima zaidi ya 190,000 wakinufaika.

Urio alisema mafanikio hayo yamechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 1.28 mwaka 2020 hadi tani milioni 2.36 mwaka 2024, jambo linaloonyesha mafanikio ya uwekezaji uliofanywa katika sekta ya kilimo na maendeleo ya wananchi mkoani Kilimanjaro.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.