WAZAZI WATAKIWA KUWA KARIBU NA WATOTO WAO ILI KUIMARISHA MAADILI NA UZALENDO

MOSHI-KILIMANJARO.

WAZAZI na Walezi wametakiwa kutenga muda wa kuwa karibu na watoto wao na kuzungumza nao mara kwa mara ili kuhakikisha wanapata malezi bora yenye maadili mema, pamoja na kutambua umuhimu wa amani, umoja na mshikamano katika jamii.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Elimu, Malezi na Mazingira wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Alhaji Ally Pendo, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya ya Wazazi yaliyofanyika katika Kata ya Njoro, wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Maadhimisho hayo yalikuwa na kaulimbiu isemayo “Malezi Bora na Uzalendo ni Msingi wa Taifa.”

Alhaji Pendo alisema changamoto ya majukumu mengi kwa wazazi imekuwa ikiwafanya kushindwa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa watoto wao, hali ambayo inaweza kuathiri malezi, maadili na hata kupunguza uzalendo kwa taifa.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa malezi bora kwa watoto ili kuwaepusha na vitendo vya kihalifu, matumizi mabaya ya dawa za kulevya pamoja na kujiingiza katika makundi mabaya yanayoweza kuharibu maisha yao ya baadaye.

Aidha alisema wazazi wanapaswa kuwa karibu zaidi na watoto wao ili kuwafahamu vizuri na kuwapa mwongozo sahihi unaoendana na mazingira ya sasa, hususan katika kipindi hiki cha ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya kijamii.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, alisema malezi bora ndiyo msingi wa mafanikio ya mtoto na taifa kwa ujumla, huku akiwataka wazazi na walezi kuweka kipaumbele katika malezi na makuzi ya watoto badala ya kujikita zaidi kwenye shughuli za kiuchumi pekee.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.