MOSHI-KILIMANJARO.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Moshi, Theresia Komba, amewataka wanawake kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii kwa kuanzia ngazi ya familia, huku akisisitiza umuhimu wa kutenga muda kwa ajili ya malezi na ustawi wa watoto.
Theresia aliyasema hayo Aprili 7, mwaka huu, wakati alipokuwa akitoa salamu za UWT katika Maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya ya Wazazi, yaliyofanyika Kiwilaya Kata ya Njoro Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro huku yakiwa na kauli mbiu ya “Malezi Bora na Uzalendo ni Msingi wa Taifa,”
Alisema Wanawake wana nafasi kubwa katika kujenga maadili mema kwa watoto na familia kwa ujumla, hivyo wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa upendo, mshikamano na mawasiliano mazuri ndani ya familia ili kuimarisha malezi bora.
Alisema changamoto nyingi zinazojitokeza katika jamii kwa sasa, zinachangiwa na kupungua kwa muda wa wazazi kukaa pamoja na watoto wao, hali inayosababisha baadhi ya watoto kukosa maadili na mwelekeo sahihi wa maisha.
Aidha, aliwahimiza Wanawake kushirikiana na waume zao katika malezi ya watoto na kuhakikisha familia zinakuwa sehemu salama ya kujifunza maadili, heshima na uwajibikaji, ili kujenga kizazi chenye nidhamu na manufaa kwa taifa.












