ULIPAJI ADA CCM WAWEKWA MBELE KATIKA WIKI YA JUMUIYA YA WAZAZI MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO.

MKUMBE wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitokea mkoa wa Kilimanjaro Said Sultani Mdeme, amesisitiza umuhimu wa wanachama wa CCM kulipa ada za uanachama kila mwaka kwa wakati, akisema hatua hiyo ni msingi wa kuimarisha chama na jumuiya zake.

Mdeme amesema hayo Aprili 7, 2026 wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya ya Wazazi kiwilaya yaliyofanyika Kata ya Njoro, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo viongozi mbalimbali wa CCM na jumuiya zake walihudhuria.

Amesema wanachama hawapaswi kusubiri kipindi cha uchaguzi ndipo wakumbuke kulipa ada, bali wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza wajibu huo ili kukiwezesha chama kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi.

“Dhima ya Jumuiya ya Wazazi ni kushiriki katika kujenga taifa kupitia chama, katika wiki hii tunafanya tathmini ya jumuiya na chama kwa kuangalia idadi ya wanachama, uhamasishaji wa wanachama wapya pamoja na ulipaji wa ada,” amesema Mdeme.

Aidha amesema lengo la maadhimisho hayo ni kufanya uhamasishaji wa shughuli za chama na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanachama kupitia shughuli mbalimbali za kijamii.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Diwani wa Kata ya Njoro, Zuberi Kidumo, amesema nguvu ya CCM inatokana na uimara wa jumuiya zake ikiwemo Jumuiya ya Wazazi, UVCCM na UWT, hivyo kuna umuhimu wa kuziimarisha zaidi.

Katika maadhimisho hayo, Kidumo alichangia kiasi cha shilingi milioni 1.8 kwa ajili ya ununuzi wa vitenga vya kushonea sare viongozi wa Jumuiya ya Wazazi kutoka kata zote 21 za Wilaya ya Moshi, wakiwemo Wenyeviti,Makatibu na Kakatibu wa Malezi, kwa kutambua mchango wao katika kukijenga chama.

Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi, Theresia Komba, amewataka Wanawake kuwa chachu ya mabadiliko kuanzia ngazi ya familia kwa kutimiza wajibu wao katika malezi na kutenga muda kwa ajili ya familia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Moshi, Edward Mangesho, amesema sababu ya kufanya Maadhimisho hayo katika Kata ya Njoro ni kutokana na Kata hiyo kuonyesha ushirikiano mkubwa ndani ya chama.

“Kata ya Njoro imeonyesha mshikamano na ushirikiano mkubwa katika shughuli za chama, jambo ambalo ni mfano wa kuigwa katika kukijenga CCM,” amesema Mangesho.

Jumuiya ya Wazazi ya CCM huadhimisha wiki hiyo nchi nzima kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo usafi wa mazingira, upandaji miti, utoaji misaada katika vituo vya afya na shule pamoja na utoaji wa elimu ya malezi bora.

Maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na Kauli Mbiu isemayo, “Malezi Bora na Uzalendo ni Msingi wa Taifa.”









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.