BARAZA LA MADIWANI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA SIHA LAMPONGEZA MKURUGENZI KWA UKUSANYAJI WA MAPATO

SIHA-KILIMANJARO 

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha limempongeza Mkurugenzi Mtendaji Hellen Emanuel Mwambeta, pamoja na Wataalamu wake kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa ipasavyo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akisoma taarifa katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Duncan Urassa, alisema hadi kufikia Machi 31, 2026, halmashauri hiyo, imekusanya Shilingi Bilioni 2.76 za mapato ya ndani, sawa na asilimia 81 ya makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, alisema halmashauri imechangia Shilingi milioni 790.21 katika miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 88.48 ya bajeti ya miradi inayotokana na mapato ya ndani.

“Nimpongeze Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha na Wataalamu wake kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuelekeza asilimia inayotakiwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alisema Urassa.

Pamoja na pongezi hizo, Mwenyekiti huyo aliuagiza uongozi wa halmashauri ya Siha, kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ili kufikia asilimia 100 au zaidi ya makadirio ya bajeti.

Aliongeza kuwa halmashauri imepokea Shilingi Bilioni 7.99, sawa na asilimia 61.29 ya fedha za miradi ya maendeleo zilizotarajiwa kupokelewa katika mwaka huu wa fedha.

Urassa aliwataka Mkurugenzi na Wataalamu kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia ubora uliokusudiwa na thamani ya fedha za Serikali.

Katika hatua nyingine, Urassa, alisema mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao, upatikanaji wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo.

Alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk. Christopher Timbuka, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuwezesha upatikanaji wa tani 52 za mbolea ya ruzuku pamoja na tani 34 kutoka kwa wadau wengine, hatua iliyosaidia kupunguza uhaba wa pembejeo hiyo.

Katika hotuba yake hiyo ambayo alitumia dakika 10, Urassa pia aliwataka maafisa kilimo wa wilaya, kata na vijiji kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, ikiwemo mbolea za asili na zile zinazopatikana kwa urahisi katika maeneo yao.

“Niwatake wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo ili mvua hizi ziweze kuleta tija katika uzalishaji,” alisisitiza.

Aidha, alisema halmashauri ya Siha,  imetoa jumla ya hati miliki 185 kwa wananchi wa vijiji vya Ormelili, Kilingi na Sanya Juu, huku zoezi la upimaji na upangaji likiendelea katika kijiji cha Munge sambamba na uhamasishaji katika maeneo mengine.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.