MOSHI-KILIMANJARO.
WATAFITI wa masuala ya mazingira kutoka nchini Marekani wamewasili Manispaa ya Moshi kwa ajili ya kufanya tathmini ya awali kuhusu uwezekano wa kulifunika dampo la zamani la taka lililopo Kata ya Kaloleni, ambalo lilifungwa baada ya kujaa taka na kutajwa kuwa hatari kwa afya ya mazingira na jamii inayolizunguka.
Hatua hiyo inalenga kupunguza madhara ya kimazingira yanayoweza kusababishwa na dampo hilo, ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa mazingira, vyanzo vya maji na athari kwa viumbe hai.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake baada ya kuupokea ugeni huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Kidumo, amesema Watafiti hao wako katika hatua za awali za kufanya utafiti utakaobaini uwezekano wa kulifunika dampo hilo kwa njia salama na rafiki kwa mazingira.
Alisema lengo kuu la utafiti huo ni kulinda afya za wananchi pamoja na kuhifadhi mazingira yanayozunguka eneo hilo, hususan kutokana na uwepo wa msitu wa asili wa Rau na vyanzo mbalimbali vya maji vilivyo karibu na dampo hilo.
“Katika eneo hilo kuna msitu wa asili wa Rau pamoja na vyanzo vya maji kama chemichemi za Goa na Liwali, ambavyo hutegemewa kwa shughuli za kilimo cha mpunga, mbogamboga na matumizi ya majumbani, hivyo uchafuzi wa mazingira unaweza kuhatarisha maisha ya viumbe hai na usalama wa maji hayo,” alisema Mhandisi Kidumo.
Alieleza kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, uchafuzi unaoweza kutokana na dampo hilo unaweza kuathiri mfumo wa ikolojia wa eneo hilo pamoja na afya za wananchi wanaotegemea vyanzo hivyo vya maji.
Meya Kidumo alisema ameridhishwa na ujio wa watafiti hao, akieleza kuwa ni hatua muhimu yenye mchango mkubwa katika juhudi za kuhifadhi mazingira na kuimarisha ustawi wa jamii.
Aidha, alisema Manispaa ya Moshi ina matumaini makubwa kuwa matokeo ya utafiti huo, ambayo yatafungua njia ya utekelezaji wa mradi wa kulifunika dampo hilo kwa viwango vinavyokubalika kitaalamu ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza kwa sasa na siku zijazo.















