TANZANIA YAANDIKA HISTORIA KUPITIA UTALII WA JIOLOJIA

DODOMA-TANZANIA.

TANZANIA imeandika historia mpya barani Afrika baada ya kuwa nchi ya pili kupata hadhi ya UNESCO Global Geopark kupitia Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai, hatua inayodhihirisha ubora wa urithi wa asili na jiolojia uliopo nchini.

Kutokana na mafanikio hayo, Serikali imejenga Makumbusho ya Kisasa ya Jiopaki (Geopark Museum) katika Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, yaliyolenga kutoa elimu kuhusu sayansi ya miamba, volkano na historia ya mazingira sambamba na kukuza utalii wa kielimu.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo bungeni Dodoma, ambapo alieleza kuwa makumbusho hayo ni ya kipekee katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alisema kupitia makumbusho hayo, Watalii na wadau mbalimbali hupata nafasi ya kujifunza historia ya dunia, maumbile ya Bonde la Ufa, pamoja na kujionea mwamba wenye umri wa zaidi ya miaka milioni tatu uliopo katika hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro-Lengai.

Aidha alisema wageni wanaotembelea eneo hilo hupata fursa ya kujifunza tamaduni za makabila ya Wahadzabe, Wairaq Wadatoga na Wamasai, sambamba na kushiriki shughuli mbalimbali za kielimu na burudani zinazotolewa ndani ya makumbusho hayo.

Makumbusho hayo yanasimmiwa na Ngorongoro Conservation Area Authority chini ya Ngorongoro Conservation Area ambayo inatambuliwa na UNESCO kwa hadhi tatu ikiwemo Eneo la Hifadhi ya Mazingira na Binadamu, Urithi wa Dunia wa Asili na Utamaduni pamoja na UNESCO Global Geopark.

Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, Tanzania ni nchi ya pili Afrika kupata hadhi hiyo baada ya Morocco, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda na kuenzi maeneo ya urithi wa taifa ili kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya uchumi.

Tanzania ina jumla ya maeneo 158 ya malikale, huku maeneo saba yakitambuliwa rasmi kuwa urithi wa dunia na UNESCO.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.