MANISPAA YA MOSHI YASAINI MKATABA WA SHILINGI BILIONI 2.1 UJENZI WA UWANJA WA MPIRA MAJENGO

Mstahiki Meya Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, akisaini Mkataba wa Shilingi Bilioni 2.1 kwa ajiki ya ujenzi wa Uwanja wa mpira wa Majengo.

MOSHI-KILIMANJARO.

HALMASHAURI  ya Manispaa ya Moshi imesaini mkataba wa shilingi bilioni 2 nukta 1 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu katika Kata ya Majengo Awamu ya Pili.

Mkataba huo umesainiwa leo Aprili 15, 2026, kati ya Manispaa hiyo na Kampuni ya SIB Stone Company Limited ya Kibaha mkoani Pwani, huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa na kuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji zaidi ya elfu 15.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, Shaban Mchomvu, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Godfrey Mnzava, amesema mradi huo utasaidia kukuza sekta ya michezo pamoja na kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema ujenzi wa uwanja huo umetokana na fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON, ambapo Moshi inalenga kuwa kituo cha timu zitakazokuja kufanya mazoezi.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Kidumo, alimtaka mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Mkandarasi wa mradi huo, Joseph Mrema, ameahidi kukamilisha kazi ndani ya muda wa mkataba huku akiomba ushirikiano kutoka kwa viongozi na wananchi.

Madiwani wa Halmashauri hiyo, Hamphrey Mosha, Khalid Shekoloa na Haruna Mushi, walisema uwanja huo utasaidia kuongeza mapato ya halmashauri pamoja na kutoa ajira kwa vijana kupitia shughuli mbalimbali zitakazoambatana na uwepo wa uwanja huo.

Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kilimanjaro, Abdallah Thabit, ameishukuru Serikali kwa kuridhia utoaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo nchini.

Alisema ujio wa timu mbalimbali za mpira wa miguu kufanya mazoezi Moshi wakati wa mashindano ya AFCON utafungua fursa kubwa ya utalii wa michezo, ambapo wageni hao pia watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo Mlima Kilimanjaro.


















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.