WATAALAMU WA AFYA TAKRIBANI 800 WAZALISHWA NA CITY INSTITUTE OF HEALTH

MOSHI-KILIMANJARO.

WATAALAMU  wa afya takribani 800 wamezalishwa na Taasisi ya City Institute of Health Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za afya nchini kupitia ongezeko la wataalamu wenye ujuzi katika hospitali na vituo vya afya.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa taasisi hiyo, Nuran Mwasha, aliyasema hayo  Aprili 15,2026 mjini Moshi, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa Wakuu wa shule za sekondari mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mashindano ya UMISSETA.

Alisema kuwa serikali imeendelea kujenga vituo vingi vya afya nchini, hivyo kuna haja ya kuhakikisha uwepo wa wataalamu wa kutosha ili kuendana na ongezeko la miundombinu hiyo ya afya.

“Tunaendelea kuiunga mkono serikali kwa kuzalisha wataalamu mbalimbali wa afya wakiwemo madaktari na wafamasia watakaosaidia kuongeza nguvu kazi katika hospitali na vituo vya afya vinavyoendelea kujengwa nchini,” alisema.

Mbali na kuzalisha wataalamu wapya, amesema taasisi hiyo pia imeendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya waliopo kazini ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika vituo vya afya na kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi wa afya nchini.

Mwasha alisema taasisi hiyo pia imekuwa mstari wa mbele kusaidia sekta ya elimu kwa kutoa vifaa vya michezo pamoja na vifaa vya kufundishia kwa shule za msingi na sekondari, huku lengo kubwa likiwa ni kuinua kiwango cha elimu na michezo nchini.

“Leo tumekabidhi vifaa vya michezo zikiwemo jezi na mipira kwa wakuu wa shule za sekondari Tanzania mkoa wa  Kilimanjaro (TAHOSSA), kwa ajili ya mashindano ya UMISSETA, lengo likiwa ni kuendelea kunyanyua michezo hapa nchini,” alisema Mwasha.

Aidha alisema taasisi hiyo imeweka utaratibu wa kuzizawadia shule zitakazowezesha wanafunzi wengi kujiunga na taasisi hiyo, ambapo kila shule itakayofanikiwa kupeleka wanafunzi watano kujiunga na City Institute of Health itapatiwa laptop tano pamoja na mashine ya photocopy.

Alieleza kuwa msaada huo unalenga kuziwezesha shule kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia ya kidigitali pamoja na kusaidia utunzaji wa siri za mitihani katika shule husika.

“Dunia ya sasa inakwenda kidigitali, lakini baadhi ya shule bado hazina vifaa vya kutosha. Kama taasisi tumeona umuhimu wa kusaidia upande huo ili kuwezesha mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji,” amesema.

Mwasha alifafanua kwamba taasisi ya City Institute of Health Dar es Salaam inatoa mafunzo katika kada mbalimbali za afya zikiwemo Clinical Medicine, Pharmaceutical Sciences, Diagnostic Therapy, Health Record and Information Technology pamoja na Social Work.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.