MANISPAA YA MOSHI YAANZA KUWEKA TAA ZA SOLA BARABARANI KUIMARISHA ULINZI

MOSHI-KILIMANJARO.

KAMPINI ya ujenzi ya Mawanjeni Electrical Services Ltd ya Dar es Salaam imeanza kufunga taa za barabarani zinazotumia nishati ya jua katika barabara mbalimbali za Manispaa ya Moshi, hatua inayolenga kuimarisha usalama na ulinzi kwa wananchi nyakati za usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo, amesema uwekaji wa taa hizo unafanyika katika barabara zote zilizopo katikati ya mji pamoja na kata zilizoko pembezoni mwa manispaa hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za halmashauri kuboresha huduma za kijamii na maendeleo ya miundombinu.

Mhandisi Kidumo amesema lengo la mradi huo ni kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara, wafanyabiashara pamoja na wananchi wanaotoka na kuingia ndani ya mji wa Moshi nyakati za usiku. 

Amesema taa hizo za sola zitasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu, ajali pamoja na changamoto ya giza iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Moshi akiwemo Musllin Hoza, Michael Uron na Elia Chamzuri wameishukuru halmashauri kwa hatua hiyo, wakisema kuwa uwekaji wa taa hizo utasaidia kuongeza usalama wa wananchi na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi nyakati za usiku. 

Wakazi hao wamesema kwa muda mrefu baadhi ya maeneo yalikuwa na changamoto ya giza hali iliyokuwa ikichangia matukio ya uhalifu na kuwafanya wananchi kutokuwa huru kufanya shughuli zao baada ya jioni.

Naye mkazi wa Kata ya Majengo Vicent Damas kwa jina maarufu (Kisisi), amesema mradi huo ni wa muhimu kwa maendeleo ya mji wa Moshi na ameitaka hManuspaa hiyo, kuendelea kusimamia uwekaji wa taa hizo ili kuhakikisha maeneo yote yanapata huduma hiyo muhimu kwa manufaa ya wananchi wote.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.