MADIWANI MOSHI WARIDHISHWA NA UJENZI WA STANDI YA KIMATAIFA NGANGAMFUMUNI

MOSHI-KILIMANJARO.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, likiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, limetembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Kimataifa cha Ngangamfumuni na kueleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kimkakati.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE), umefikia asilimia 68 ya utekelezaji wake, huku ukitajwa kuwa miongoni mwa miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Manispaa ya Moshi na maeneo jirani.

Wakizungumza baada ya kutembelea mradi huo, baadhi ya madiwani akiwemo Diwani wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, alisema wamefarijika kuona mradi huo uliokuwa umekwama kwa muda mrefu sasa ukiendelea kwa kasi kubwa chini ya mkandarasi huyo.

Shekoloa alisema kukamilika kwa standi hiyo kutafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa Moshi, hasa wafanyabiashara, wamiliki wa mabasi pamoja na wajasiriamali wadogo na wa kati.

“Tumefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa standi mpya ya mabasi ya Ngangamfumuni, mradi huu utakapokamilika utakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwa wananchi wa Moshi na wafanyabiashara mbalimbali watanufaika kwa kiwango kikubwa,” alisema Shekoloa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mfumuni, Stewart Nathaniel, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kusimamia mradi huo hadi kufikia hatua ya sasa baada ya kusuasua kwa muda mrefu.

Alisema kituo hicho kikikamilika kitasaidia kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi sambamba na kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafiri kwa wakazi wa mji huo.


Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Manispaa ya Moshi, Daniel Kileo, alisema Serikali Kuu imetoa shilingi bilioni 8.2 huku Manispaa ikichangia shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo.

Alisema mkandarasi tayari amelipwa fedha za awali kiasi cha shilingi bilioni mbili, na kufanya jumla ya fedha zilizokwisha kutolewa kufikia shilingi bilioni 10.7 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

“Kiasi cha jumla ya shilingi bilioni 19.7 kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha mradi huu. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha za kuhakikisha mradi huu unakamilika,” alisema Kileo.

Awali, Mhandisi wa mradi huo, Ibrahim Nkya, alisema endapo fedha zilizobaki zitatolewa kwa wakati, ndani ya miezi mitatu mradi huo utakuwa umekamilika na tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Kidumo, alisema ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya mradi huo wa kimkakati na kuhimiza kasi zaidi ya utekelezaji wake.

“Tunaishukuru Serikali Kuu kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za maendeleo ndani ya Manispaa yetu. Tunamtaka mkandarasi kuongeza kasi ili mradi huu ukamilike na kukabidhiwa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu,” alisema Kidumo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Uhuru Mwembe, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zake.

Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa wakati uliopangwa ili kuwanufaisha wananchi.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.