DIWANI, WANAFUNZI WALAZIMIKA KUCHOTA MAJI YA MTONI KUTOKANA NA MUWSA KUSHINDWA KUWAPELEKEA HUDUMA YA MAJI

MOSHI-KILIMANJARO.

WANAFUNZI wa Shule za Msingi Samanga na Mlokola, Wilaya ya Moshi Vijijini, wanalazimika kuchota maji mtoni kufuatia ukosefu wa huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, Diwani wa Kata ya Marangu Mashariki, Innocent Shirima, amesema hata yeye hulazimika kwenda kuchota maji pamoja na wanafunzi, jambo ambalo ni hatari kiafya huku alionya kuwa hali hiyo inaongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

Shirima ameitoa rai kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, akipendekeza iwapo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imeshindwa, basi jukumu hilo lipelekwe kwa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).

Amesema kuwa licha ya Kata hiyo kuwa na vyanzo na chanzo cha maji cha Lyasongoro, bado wananchi wa kata hiyo hawapati maji ya uhakika, huku akidai kuwa hali ya upatikanaji wa maji ilizorota zaidi baada ya MUWSA kuanza kusimamia huduma hiyo.

Wakichangia taarifa hiyo ya maji baadhi ya madiwani akiwemo Diwani wa Kata ya Kindi, Samwel Kirumbuyo, amesema wananchi wa maeneo ya Sambarai na kitongoji cha Eka wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.

Naye Diwani wa Viti Maalum Kata ya Njia Panda, Mese Mndeme, amesema kuwa licha ya uhaba wa maji, wananchi wamekuwa wakitozwa bili kubwa na wakati mwingine kukumbana na lugha zisizofaa kutoka kwa watumishi wa MUWSA.

Diwani wa Kata ya Old Moshi Mashariki, James Lyimo, amesema kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha, bado wananchi wanapata mgao wa maji, hali ambayo haikuwahi kushuhudiwa hapo awali.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi Vijijini, John Mapato Meela, alikiri kuwepo kwa changamoto katika chanzo cha Lyasongoro na kusema tayari maagizo yalishatolewa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, kwa MUWSA kuunda timu ya wataalamu kuchunguza tatizo hilo.

Alimtaka Afisa Uhusiano wa MUWSA kuhakikisha taarifa hiyo anaiwasilisha kwa Mkurugenzi wa MUWSA ili hatua zichukuliwe haraka na majibu yawasilishwe katika kikao kijacho cha robo ya nne.

Akijibu hoja hizo, Afisa Uhusiano wa MUWSA, Florah Nguma, amesema Mamlaka hiyo inatoa huduma katika vijiji vinne vilivyoko Kata ya Marangu Mashariki na kwamba kuna mradi unaotekelezwa katika chanzo cha Lyasongoro ili kuboresha upatikanaji wa maji.

Amesema kwa sasa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo ikiwemo Samanga inatolewa kwa mgao kutokana na hali ya upatikanaji wa maji katika vyanzo husika.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.