BODI YA KAHAWA TANZANIA YAENDELEA KUWA KINARA WA KAHAWA AFRIKA MASHARIKI

MOSHI-KILIMANJARO.

BODI ya Kahawa Tanzania (TCB) imesema inaendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa sekta ya kahawa na kudumisha ubora wa zao hilo, hali inayoiweka Tanzania kuwa kinara wa kahawa hususan Arabika katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Moses Simwinga, wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika Kimkoa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), mkoani Kilimanjaro.

Simwinga amesema Bodi ya Kahawa inajivunia kushiriki moja kwa moja katika kuwahudumia wakulima wa kahawa kwa kuhakikisha wanapata mazingira bora ya uzalishaji na soko la uhakika.

Amesema kupitia Kaulimbiu ya bodi hiyo inayosema “Kazi Yetu ni Furaha kwa Mkulima” inaakisi dhamira ya taasisi hiyo kuhakikisha mkulima ananufaika na zao lake.

“Tunahakikisha mkulima anapata bei nzuri ya kahawa, miche bora ya kahawa chotara, pamoja na huduma za ugani zinazomsaidia kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao,” amesema Simwinga.

Aidha, ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Bodi ya Kahawa, hasa katika kusaidia upatikanaji wa taarifa kutoka Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao (AMCOS) na kuhakikisha wakulima wanapata miche bora iliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).

Amesema jitihada kubwa zinaendelea kuhakikisha wakulima katika kata na wilaya mbalimbali wanapata miche ya kahawa kwa wakati, hasa katika kipindi hiki cha mvua ili waweze kuipanda na kuongeza uzalishaji.

Kwa mujibu wa Simwinga, katika mwaka huu wa fedha bei ya kahawa imeendelea kuwa nzuri na yenye ushindani, ambapo kahawa za CPU zimefikia shilingi 12,000 kwa kilo, huku kahawa ya Arabika ikiuzwa kwa wastani wa shilingi 9,500 kwa kilo.

Amewataka wakulima kuendelea kutunza mashamba yao na kuzingatia ubora wa kahawa ili waweze kupata bei nzuri zaidi katika soko.

Simwinga amesema kupitia msaada wa Serikali Kuu na Wizara ya Kilimo, Bodi ya Kahawa imeendelea kupata ruzuku ya miche ya kahawa, hatua iliyochochea wananchi wa Kilimanjaro na Kanda ya Kaskazini kuhamasika zaidi kupanda miche hiyo.

Kutokana na hatua hizo, amesema ubora wa kahawa umeongezeka kwa kiasi kikubwa huku uzalishaji wa kahawa za CPU ukiongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Ubora wa kahawa yetu umeendelea kuimarika na Tanzania inaendelea kusimama kama kinara wa kahawa ya Arabika katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema.

Aidha, Bodi ya Kahawa imefanikiwa kufungua masoko mapya, kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta ya kahawa, jambo linalotajwa kuchangia kukuza uchumi wa taifa, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuboresha maisha ya wakulima wa kahawa nchini.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.