Mbunge wa Mwanga Dk Ngwaru Maghembe (kulia), akimkabidhi moja ya betri ya sola mganga mkuu wa wilaya ya Mwanga Dk Serijo Kusekwa wa kwanza kulia na katikati ni Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kivisini Dk Winfridi Katonji.
KIVISINI-MWANGA.
MBUNGE wa Jimbo la Mwanga, Ngwaru Maghembe, amesema atatekeleza kwa vitendo ahadi zote alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2025, huku akiwaomba wananchi kuendelea kuwa na subira wakati utekelezaji wa ahadi hizo ukiendelea.
Dk. Maghembe aliyasema hayo wakati alipokabidhi betri nne za sola katika Zahanati ya Kivisini, akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa imani yao pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza katika hafla hiyo, alisema alipokuwa akiomba kura katika Kata ya Kivisini, wananchi walimweleza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika zahanati hiyo.
Alisema betri za awali zilizokuwa zikitumia nishati ya sola zilikuwa zimeharibika na kushindwa kuhifadhi umeme, hali iliyosababisha ugumu mkubwa katika utoaji wa huduma za afya.
“Niliahidi kuleta betri mpya ili kuimarisha huduma ya umeme katika zahanati hii, na leo nimetimiza ahadi hiyo.” alisema Dk. Maghembe.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kivisini, Dk. Winfridi Katonji, alimshukuru mbunge huyo kwa kutimiza ahadi yake, akisema changamoto ya umeme ilikuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma.
Alisema mara kadhaa akina mama wajawazito walipofika kujifungua, umeme ulikatika na kuhatarisha usalama wa mama na mtoto.
Aidha, ameeleza kuwa serikali imeanzisha mfumo wa utoaji huduma za tiba kwa njia ya mtandao, hivyo kukatika kwa umeme kulikuwa kikwazo kikubwa katika utoaji wa huduma hizo.
“Unamuhudumia mgonjwa kwa kutumia mfumo wa mtandao, ghafla umeme unakatika katikati ya matibabu. Hii ilikuwa kero kubwa sana. Tunamshukuru Mbunge kwa kutuletea betri hizi ambazo zitaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.”alisema Dk. Katonji.
Aliongeza kuwa uwepo wa betri hizo utaifanya zahanati kuwa na umeme wa uhakika kupitia mfumo wa sola, tofauti na umeme wa gridi ya taifa ambao hukatika mara kwa mara.
Naye mmoja wa wakazi wa Kivisini, Bakari Mvungi, alisema baadhi ya viongozi hutoa ahadi na kushindwa kuzitekeleza, lakini Mbunge Maghembe ameonyesha mfano kwa kutimiza alichoahidi.
“Kitendo cha kutimiza ahadi hii kitaleta mwanga wa uhakika katika zahanati yetu na kuboresha huduma za afya kwa wananchi wote.” alisema.
Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa mbunge huyo wa kurejea kwa wananchi wake baada ya uchaguzi, kwa lengo la kufuatilia na kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo, hususan katika sekta za elimu, afya, maji, barabara na nishati.











