Kauli Mbiu: "Leo Yetu Ni Imara, Na Kesho Yetu Yenye Matumaini"
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Njoro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, ameibuka mshindi kwa kishindo baada ya kupata kura zote 441, bila kupoteza hata kura moja.
Mhandisi Kidumo alikuwa mgombea pekee, ambapo wajumbe wa mkutano mkuu wa kata hiyo walimpigia kura kwa kauli moja, jambo lililoonyesha wazi uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi na wanachama wa CCM katika kata hiyo.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Kidumo alisema: “Ninawashukuru wananchi wa Kata ya Njoro kwa ushirikiano mkubwa na kwa heshima kubwa ya kunipatia kura zote, bila kupoteza hata moja, hii ni heshima ya kipekee kwa wakazi wa Njoro."
Aidha, aliahidi kwenda kutekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa kwa wananchi:
“Nina deni kubwa sana la kwenda kulipa mbele ya wananchi, yale niliyoyaahidi nitayatekeleza kikamilifu, kwa kushirikiana na CCM, na kuhakikisha kila changamoto ya mwananchi inatatuliwa kwa wakati"
