AHADI TANO ZA MGOMBEA UDIWANI KATA YA MWIKA KUSINI JOHN ROBERT TARIMO; KWA WANANCHI ZAKONGA NYOYO ZA WAJUMBE


MWIKA-KUSINI.

Mgombea Udiwani wa Kata ya Mwika Kusini, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Robert Tarimo, Agosti 2, 2025, amewasilisha vipaumbele vyake vitano kwa Wajumbe wa chama hicho, katika mkutano wa chama hicho uliofanyika eneo la Ghorofani, kijiji cha kondeni, kitongoji cha kisharrini.

Katika hotuba yake, Tarimo aliahidi kushughulikia changamoto sugu zinazowakabili wakazi wa kata hiyo endapo atapewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi wa Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Alisema “Kipaumbele chake cha Kwanza; Ni kuhakikisha Kata ya Mwika Kusini inapata kituo cha afya,” alisema Tarimo na kuongeza kuwa kwa miaka mingi kata hiyo imekuwa bila huduma ya afya ya uhakika, kinyume na matakwa ya Ilani ya CCM inayotaka kila kata kuwa na kituo cha afya, ameahidi kushirikiana na Serikali pamoja na chama kuhakikisha kituo hicho kinapatikana.

Kipaumbele cha Pili  Maji, Tarimo alisema tayari ameanza kufanya utafiti wa vyanzo vya maji vilivyopo ndani ya ardhi ya Mwika Kusini. “Tayari nimebaini vyanzo vya maji, na endapo nitachaguliwa, nitashirikiana na Mamlaka husika pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha tunapata chanzo chetu cha maji na kujenga tanki kubwa litakalotatua tatizo la maji kabisa,” alieleza.

Katika kipaumbele cha Tatu, Tarimo aligusia usalama wa wakazi kwa kuahidi kusimamia upatikanaji wa kituo cha polisi katika kata hiyo kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine.

Kipaumbele cha Nne Barabara, Tarimo alisema tayari ameanza kushughulikia changamoto hiyo kwa kushirikiana na jamii katika vijiji vya Kiruweni, Mawanjeni, Kondeni na Kimangaro.

“Barabara ni kichocheo cha maendeleo, watu wanashindwa kusafirisha mazao yao kwa sababu ya barabara duni, nataka kuandika historia katika suala hili,” alisema.

Kipaumbele cha Tano; ni ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kata. Tarimo aliahidi kushirikiana na watu wenye asili ya kata hiyo wanaoishi nje ili kusaidia kujenga ofisi hiyo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Wajumbe mbalimbali wa CCM kutoka maeneo tofauti ya kata hiyo, na ulifanyika kwa utulivu huku Wajumbe wakisikiliza kwa makini na kuonyesha matumaini juu ya ahadi hizo.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.