MOSHI-KILIMANJARO.
Timu ya Matindigani FC imeandika historia ya ushindi wake wa kwanza katika hatua ya makundi ya michuano ya Zuberi Cup Tournament 2025 kwa kuichapa Kibo Worries bao 1-0, katika mchezo uliopigwa jana Julai 23, kwenye viwanja vya Railway Njoro mjini moshi mkoani hapa.
Bao
hilo pekee la ushindi lilifungwa katika dakika ya 59 ya kipindi cha pili na
nyota wa mchezo, Juma Pogba, ambaye alivaa jezi namba 11.
Pogba alionesha kiwango cha juu na mashambulizi ya kasi yaliyowaweka Kibo Worries katika wakati mgumu, na hatimaye kuibuka mchezaji bora wa mchezo huo.
Mashindano ya Zuberi Cup Tournament 2025 kwa sasa yako katika mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi, yakihusisha timu 41 zilizogawanywa katika makundi manane (8). Kila kundi lina timu tano, isipokuwa kundi F lenye timu sita.
Akizungumza Mwenyekiti wa mashindano hayo Mwl. Japheth Mpande amesema michuano hiyo ilizinduliwa rasmi Julai 19, 2025 kupitia mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya bingwa mtetezi Green Eagle na Afro Boys.
Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kabla ya Afro Boys kushinda kwa mikwaju ya penalti 6-5, kwenye mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Railway Njoro, mjini Moshi.
Hadi sasa, michezo iliyokamilika ni pamoja na Pasua Big Star 3–0 Kilimanjaro Big Star, Simbaz 0–0 Tiger, Machava 1–0 Fire.
Zuberi Cup Tournament 2025 inaendelea kuvutia mashabiki wengi, huku ushindani ukizidi kupamba moto kila siku, ambapo timu zote zinaonyesha kiu ya kuwania ubingwa, na mechi zijazo zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali zaidi.



