ZUBERI CUP YAGEUKA FURSA YA KIUCHUMI KWA AKINA MAMA NA VIJANA MOSHI

MOSHI, KILIMANJARO.

Mashindano ya soka ya Zuberi Cup yanayoendelea katika Manispaa ya Moshi yamegeuka kuwa chanzo muhimu cha fursa za kiuchumi kwa wanawake wajasiriamali na vijana, hususan wale wanaojihusisha na biashara ndogondogo viwanjani.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo uliowakutanisha Badland FC na Shirimatunda FC, uliomalizika kwa sare ya bao 1–1 kwenye uwanja wa Railway–Njoro, mkazi wa mtaa wa Sokoni Kata ya Njoro  Athumani Omari maarufu kama Semkiwa, alisema kuwa mashindano hayo yamekuwa mkombozi mkubwa kwa jamii ya Moshi.

“Wanawake wengi wamekuwa wakitumia fursa hii kuuza bidhaa zao kama uji, juice, mandazi, vitafunwa na ubuyu, vijana nao wamekuwa wakileta viti kwa ajili ya watazamaji na kutoza ada ya shilingi 500 kwa kiti, kwa hakika ni mashindano ya michezo lakini pia ya kimaendeleo,” alisema Semkiwa.

Mchezo huo ulikuwa sehemu ya hatua za makundi ya awali ya Zuberi Cup 2025, ambayo mwaka huu yanashirikisha timu 41 kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Moshi, ambapo tangu kuanzishwa kwake miaka mitano iliyopita na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Njoro, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, mashindano haya yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji na kuinua uchumi wa watu wa kawaida.

“Napenda kumpongeza Mhandisi Zuberi kwa moyo wake wa kizalendo, ametusaidia sana, si tu kwa kuanzisha mashindano haya, bali pia kwa kuuboresha uwanja kwa kupanda nyasi nzuri, sasa vijana wanafurahia kucheza kwenye mazingira rafiki na salama,” aliongeza Semkiwa.

Kwa upande mwingine, mdhamini wa mashindano hayo kupitia kampuni ya mavazi ya Yusco Chimbo Collection, Yusuph Abduel, alieleza kuwa ushiriki wao unatokana na imani waliyonayo kwa vijana na mapenzi ya michezo.

“Vijana wanapenda michezo na pia hutununuza bidhaa zetu, hivyo kuunga mkono mashindano haya ni njia ya kurudisha kwa jamii, tunatamani kuona vijana wanapata nafasi ya kukuza vipaji vyao lakini pia kuinuka kiuchumi kupitia fursa hizi,” alisema Abduel.

Zuberi Cup imekuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Moshi na maeneo ya jirani, huku maelfu ya watu wakijitokeza kila siku kushuhudia mechi, jambo ambalo linachochea mzunguko wa fedha na maendeleo ya biashara za mitaani.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.