MADAKTARI BINGWA KUTOKA MUHIMBILI KUTIBU BURE MOSHI: AFYA YA AKILI YAZIDI KUWA CHANGAMOTO KWA VIJANA

MOSHI-KILIMANJARO.

Matatizo ya afya ya akili yameendelea kuwa tishio miongoni mwa vijana duniani, huku wataalamu wakibainisha kuwa chanzo kikuu ni msongo wa mawazo, matumizi ya pombe na mihadarati.

Takwimu zinaonesha kuwa kujiua kunashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo vya vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19, hali inayoashiria ukubwa wa tatizo hilo.

Kutokana na changamoto hizo, timu ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imewasili katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuendesha kambi maalum ya matibabu ya bure kuanzia Julai 25 hadi Julai 27, 2025, katika viwanja vya Uhuru Park, Moshi mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Aika Shoo, Daktari Bingwa wa Watoto kutoka Muhimbili, alisema kuwa kambi hiyo inalenga kuwahudumia wananchi wa makundi maalum, ikiwemo watu wenye ulemavu na wale wanaokumbwa na changamoto za afya ya akili.

"Tutakuwa tunatoa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya ya wanawake, macho, meno, magonjwa ya afya ya akili, saratani, watoto, lishe, pamoja na magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Dkt. Shoo.

Dkt. Shoo aliongeza kuwa lengo ni kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,700 katika kipindi cha siku hizo tatu, kuanzia saa kumi na moja alfajiri kila siku.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo za bure, akisisitiza kuwa ujio wa madaktari hao ni fursa adhimu kwa wananchi kupata tiba kwa magonjwa mbalimbali bila malipo.

“Ujio wa kambi hii ya madaktari bingwa wa Mama Samia kutoka Muhimbili, kwa kushirikiana na Vodacom Foundation, utakuwa chachu kwa wananchi kupata matibabu bure. Niwaombe wananchi kujitokeze kwa wingi,” alisema RC Babu.

Naye Meneja wa Vodacom mkoa wa Kilimanjaro, Sifa Msua, alisema kuwa kampuni hiyo kupitia Vodacom Foundation imejikita kusaidia sekta mbalimbali nchini, na safari hii wameamua kuwekeza kwenye afya kwa lengo la kurejesha kwa jamii kile wanachopokea.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.