UWT-SIHA; YAWATAKA MADIWANI VITI MAALUMU KUWA CHACHU YA MAENDELEO KWA WANAWAKE

SIHA-KILIMANJARO.

Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro, umewataka madiwani watakaopatikana kupitia kura za maoni kwa nafasi za viti maalum kuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake, kushirikiana na halmashauri katika kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inawafikia walengwa, na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kauli hiyo imetolewa Julai 20,2025 na Katibu wa UWT Wilaya ya Siha, Mwanaidi Kaleghela, wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa UWT uliofanyika leo katika Ukumbi wa (RC-Hall), kwa ajili ya kupiga kura za maoni kuwachagua wanawake wanaowania nafasi za udiwani kupitia viti maalum.

“Ninawapongeza wajumbe kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mchakato huu muhimu, tuna imani kuwa madiwani watakaochaguliwa watakuwa sauti ya wanawake na chombo cha maendeleo katika wilaya yetu,” alisema Kaleghela.

Kaleghela alisisitiza kuwa madiwani hao wanapaswa kushirikiana kikamilifu na UWT katika kusimamia upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotolewa na halmashauri, pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na uwajibikaji na matokeo chanya ya kiuchumi kwa wanawake.

Aidha, alitoa wito kwa viongozi hao wapya kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kusimamia haki za wanawake katika jamii.

Katika mchakato huo, wanawake 20 waliwasilisha nia ya kugombea nafasi ya udiwani kupitia viti maalum, ambapo 15 walipitishwa kuwania nafasi hiyo, kupitia mkutano huo, wajumbe wanatakiwa kuwachagua wagombea sita (6) kati ya hao 15, ambao wataiwakilisha Wilaya ya Siha katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Wajumbe waliotarajiwa kushiriki katika mchakato huo ni 822, lakini walioweza kuhudhuria na kushiriki zoezi la upigaji kura ni 794, idadi ambayo ilionyesha muitikio mkubwa na wa kujivunia kwa upande wa jumuiya hiyo.

Akifungua rasmi mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha, Wilfred Moshi, aliwataka wajumbe kuhakikisha wanachagua viongozi bora, waliokomaa kisiasa na wenye uwezo wa kuiwakilisha vema jumuiya hiyo katika baraza la madiwani.

“Kura zenu ni msingi wa ushindi wa chama chetu, ifikapo Oktoba mwaka huu, tunatarajia kila kura ya mwanachama iwe kwa Rais Samia Suluhu Hassan, huku akisema kuwa shindi wa madiwani ni asilimia 40 ya mafanikio ya CCM,” alisema Moshi,"alisema.

Pia alihimiza wajumbe na wanachama wa CCM kuhakikisha kata zote 17 zilizopo wilayani Siha zinachukuliwa na chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao, kama sehemu ya mkakati wa kulinda na kuendeleza maendeleo yaliyopatikana.
















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.