NEEMA YAWASHUKIA WAKULIMA WA MPUNGA SKIMU YA UMWAGILIAJI MAWALA-MOSHI


MOSHI-KILIMANJARO.

Wakulima wa zao la mpunga wa eneo la Mawalla wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wanatarajiwa kuongeza kipato chao kinachotokana na zao hilo kutokana na mpango ulioanzishwa wa kuongeza thamani ya zao hilo.

Hayo yameelezwa Julai 18,2025 na Mwenyekiti wa Taasisi ya isiyo kuwa ya kiserikali ya Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK) Jaffari Ally wakati wa utiaji saini (MoU) kati ya taasisi hiyo na uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Moshi, utaopelekea kuanzishwa kwa mradi wa kuongeza thamani zao la mpunga.

Alisema mradi huo utahusisha ujenzi na usimikaji wa mashine ya kukoboa mpunga katika kijiji cha Mawala Kata ya Kahe Magharibi, Wilaya ya Moshi, mkoani hapa.

Ally alisema kuwa kuanzishwa kwa mradi huo pia utawaondola adha ya wakulima wa eneo hilo kusafiri mwendo mrefu Kwenda kukoboa mpunga kabla ya kuuza au matumizi mengine.

“Eneo la mradi wa Mawala na Kata ya Kahe Mashariki kwa ujumla, kuna mradi wa umwagiliaji ambao unaendeshwa chini ya (Ongama) vijiji vya Oria, Ngasini na Mawala; wakulima wa eneo hili huzalisha mpunga mwingi lakini mapato yao yalikuwa ni duni kutokana na kukosa miundombinu ya kuongeza thamani ya mpunga wanaozalisha”, alisema.

Aliongeza, “Kuanzishwa kwa mradi huu utawawezesha kuongeza thamani ya zao la mpunga na hivyo kuboresha maisha yao na pia kuimarisha kilimo cha mpunga”.

Aliendelea kusema kuwa mradi huo ni sehemu ya miradi mingi ambayo FTK inafanya kwa ushirikiano na serikali kupitia halmashauri ya Wilaya ya Moshi yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kukuza pato la wilaya.

“Tunafanya kazi kwa kusaidiana na Serikali, kupitia halmashauri ya Wilaya ya Moshi pamoja na halmashauri zingine zinazopakana na Kampuni ya uzalishaji wa sukari TPC, ambazo ni pamoja na Wilaya ya Hai, iliyoko mkoani Kilimanjaro na Wilaya ya Simanjiro iliyoko Mkoa wa Manyara”, alisema.

Aliendelea kusema kuwa miradi hiyo ni pamoja na ile ya sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara, miradi ya umwagiliaji pamoja na uboreshaji na uhifadhi wa mazingira.

Akiongea katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mhandisi Fridolin Mpanda, aliushukuru uongozi wa TPC na ule wa FTK kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika halmashauri hiyo ambayo alisema imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya wananchi wa wilaya hiyo.

Akizungumzia mradi huo, Mhandisi Mpanda alisema utakuwa mkombozi wa wananchi wa kijiji cha Mawala ambao alisema walikuwa wakitembea mwendo mrefu kutafuta huduma za kuboresha mazao yao kila msimu.

Naye Mtendaji msaidizi wa FTK Kuya Nangai, alisema mradi huo utachangia pamoja na mambo mengine kuongezeka kwa fursa za ajira kwa wananchi wa eneo la mradi huo.

“Ajira hizo ni za moja kwa moja kwenye mradi wenyewe na eneo la kujiajiri kutokana na ukweli kuwa kuweko kwa mradi huo wa kuongeza thamani ya zao la mpunga utachochea vijana wengi kujiunga na kilimo cha mpunga ili kujipatia mapato”, alisema.

Mkazi wa kijiji cha Mawala Kibaru Kimani, alisema ujenzi wa kiwanda cha kukoboa mpunga kitakwenda kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu.

"Tulikuwa tuna vuna mpunga na kuusafirisha kwa gharama kubwa umbali wa kilomita zaidi ya 10 kwa ajili ya kuukoboa; kiwanda hiki kitatupunguzia gharama za umbali ambapo hadi kufika mjini kuliko kiwanda cha kukobola tulikuwa tunatumia Sh 5,000/- kwa gunia moja la mpunga”, alisema.

Awali katika taarifa yake, Afisa Kilimo halmashauri ya Wilaya ya Moshi Magambo Mwongera, alisema kuweko kwa mradi huo, kutawaletea wakulima neema ya mapato ya ziada.

“Wakukima wengi wamekuwa wakipata kipato duni kwa kuuza mpunga wao bila kuukoboa kwa wafanyabiashara wa kati; sasa hivi watapata kipato zaidi kwa kuuza mazao ambayo yameongezewa thamani”, alisema. wakati wa msimu wa uvunaji, ambapo mpunga huwa na bei ya chini.

"Ujenzi na usimikaji wa mashime ya kisasa ya kukoboa mpunga utapunguza gharama za usafirishaji kwa kuwasogezea karibu huduma wananchi sambamba na kuongeza pato la mkulima, serikali na kijiji kwa ujumla,"alisema Mwongera.

Aidha alisema kuwa mradi huo umegharimu jumla ya Sh milioni 273.06 ambapo wananchi wamechangia Sh milioni 6 na kilichobakia kimegharamiwa na taasisi ya FTK.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.