MOSHI-KILIMANJARO.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo, imeanza kutekeleza mikakati ya kuboresha viwanja vya michezo kwa lengo la kuinua kiwango cha michezo katika Wilaya ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa Julai 18,2025 na mratibu wa mashindano ya mpira wa miguu ya kombe la Zuberi Cup Tournament 2025, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa tano wa mashindano hayo, yaliyofanyika katika Viwanja vya Railway vilivyopo Kata ya Njoro, Moshi Mjini.
“Mashindano ya mwaka huu yana sura mpya baada ya uwanja huu wa
Railway kufanyiwa ukarabati mkubwa ikiwemo kuwekwa nyasi na kuboresha maeneo
ambayo watazamaji wanaweza kukaa au kusimama na kuangalia mchezo bila wasiwasi
wowote wala msongamano tofauti na miaka iliyopita”, alisema Mhandisi Kidumo.
Alisema mashindano hayo mbali na kulenga kukuza na kuibua vipaji vipya, pia yamelenga kutoa burudani kwa wananchi wa Manispaa Moshi na zile kata za pembezoni.
“Watu wa Moshi ni wapenda soka; kwa vile mara nyingi husubiri michuano ya soka kupitia ligi mbalimbali, sisi waratibu wa Zuberi Cup Tourment-2025, tukaona umuhimu wa kuanda mashindano haya kila mwaka, ili kukidhi kiu yao”, alisema.
Kidumo ambaye ni Diwani Mstaafu wa kata ya Njoro halmshauri ya
Manispaa ya Moshi na pia Meya Mstaafu wa Manispaa hiyo, alisema mbali na
ukarabati wa uwanja huo, mipango ya baadaye ni kujenga uwanja kwa ajili ya
mchezo Netiboli ili wana michezo wa kike waweze kuwa na michuano yao.
“Baadaye ya ukarabati huu wa uwanja huu wa Railway nguvu kubwa tunazielekeza kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa Nelson Mandela ulioko eneo la Pasua; lengo ni kuhakikisha kunakuwa na uwanja wa michezo wa uhakika katika kila kata ya Manispaa ya Moshi”, alisema.
Akiongea kwenye hafla hiyo, Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Tarimo alisema mpango huo wa kuboresha viwanja na mkakati mahsusi unaolenga kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza michezo nchini.
“Ukarabati wa uwanja huu wa Railway ni mwendeleo wa kazi nzuri iliyofanywa ya kuboresha uwanja wa Majengo ambao sasa unaweza kutumika kwa michezo mikubwa ya mpira wa miguu”, alisema.
Kuhusu michuano ya kombe la Zuberi, Tarimo alitoa pongezi kwa waratibu wa mashindano hayo ambayo alisema inawapa moyo vijana wengi kushiriki mchezo muhimu wa soka ambao sasa umekuwa ni chanzo cha kukuza Uchumi wa wachezaji na Taifa kupitia sekta ya michezo.
“Sekta ya michezo imekuwa ni sehemu muhimu katika kukuza Uchumi tofauti na miaka yq nyuma ilipokuwa ikionekana kama sehemu ya burdani tu; na hapa nchini imeendelea kukua kwa kasi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mstari wa mbele katika kukuza sekta hii kwa kuwapa wachezaji motisha jambo ambalo linawapa moyo wa kufanya vyema zaidi”, alisema.
Tarimo alitoa pongezi kwa wandaaji wa mashindano hayo wakiongozwa na mratibu mkuu Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, pamoja na wadhamini ambao alisema ni pamoja na Benki ya Azania, Raz Builder's TanzaniaLtd, Moshi FM, Izack Enterprises, Hugo's Garden, Yusco Chimbo Collection, Halotel, na Highlife Gin , ambapo alisema ushiriki wao ni unachagia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya michezo wilayani Moshi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo Mwl. Japheth Mpande, alisema michuano ya mwaka huu itashirikisha jumla ya timu 41.
“Timu hizi 41 zimechujwa kutoka maombi ya timu 68 ya ushiriki kutoka vilabu mbalimbali; idadi hii kubwa ya maombi inadhihirisha jinsi michuano hii inavyozidi kukua na kuvutia washiriki wengi kila mwaka”, alisema.
Wakati wa hafla hiyo, mechi ya uzinduzi ilihusisha mchezo wa
ngao ya hisani kati ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Green Eagle na
washindi wa pili Afro Boys, ambapo Green Eagle ilipata ushindi kupitia mikwaju
ya penalti 5-4, baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 baada ya dakika 90 za
kawaida.
























