MEIJO LAIZER ACHUKUA FOMU YA UBUNGE JIMBO LA SIHA KUPITIA CCM

SIHA-KILIMANJARO.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Siha, Meijo Loloinyo Laizer, leo Juni 28, 2025, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wa Jimbo la Siha kupitia chama hicho.

Meijo, ambaye pia ni mmoja wa waliowahi kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoka Wilaya ya Siha, alipokelewa katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Siha saa 7:15 mchana na kukabidhiwa fomu na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya hiyo, Abdallah Chumu, kwa niaba ya Katibu wa CCM Wilaya.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Meijo alisema hatua yake ni utekelezaji wa haki yake ya kikatiba, huku akisisitiza dhamira yake ya kuleta mshikamano, umoja na kuimarisha taasisi ya Ubunge ndani ya wilaya hiyo.

“Nimefika hapa kufuata haki yangu ya kikatiba ya kugombea kwenye Jimbo la Siha, nimelelewa na CCM, naelewa misingi yake, na kama nitapata ridhaa ya chama, nitaliongoza jimbo hili kwa uadilifu mkubwa,” alisema Meijo.

Ameongeza kuwa dhamira yake kuu ni kuhakikisha kwamba heshima ya Chama Cha Mapinduzi katika Wilaya ya Siha inarejeshwa, kwa kuwa na Mbunge anayekijua, kukiheshimu na kukitumikia chama kwa weledi.

“Nia yangu ni kuwaunganisha wana-Siha wote. Mbunge anatakiwa awe na ofisi ya kutatua kero za wananchi, Si sahihi kuwa Mbunge kwa miaka 10 bila kuwa na ofisi inayojulikana, nitahakikisha kila kata na tawi lina ofisi ya chama, na sitaruhusu siasa za ukabila, udini au kanda kugawa watu wetu,” aliongeza Meijo.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, Meijo aliwahi kuwania nafasi hiyo na kushika nafasi ya tano miongoni mwa wagombea wengine waliokuwa ni pamoja na Aggrey Mwanri, Godwin Mollel, Tumsifu Kweka na Yunice Mmari.

Hatua ya Meijo kuchukua fomu inakuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kulivunja Bunge la 12, Juni 27, 2025, ikiwa ni ishara ya maandalizi rasmi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.