WAZIRI LUKUVI; MAANDALIZI YA MAZISHI YA HAYATI CLEOPA MSUYA YAMEKAMILIKA


MWANGA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. William Lukuvi, kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma, Mei 11,2025 waliwasili wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kukagua maandalizi ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Cleopa David Msuya.

Wakiwa na wajumbe na viongozi wa serikali na mkoa wa Kilimanjaro, Mawaziri hao walitembelea Uwanja wa Cleopa Msuya pamoja na nyumbani kwa marehemu, kijiji cha Usangi, na kutoa taarifa kuhusu hatua za maandalizi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Lukuvi alisema wamefika kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha maandalizi yote yanafanyika kwa heshima inayostahili.

“Mwenzangu Hamza Hassan Juma na mimi tumefika hapa kwa ajili ya kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha mzee wetu, Hayati Cleopa Msuya, anapumzishwa kwa heshima zote kama alivyoelekeza Rais,” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa ratiba, mwili wa marehemu utaagwa na Wananchi wa Wilaya ya Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro katika Uwanja wa CD Msuya, Mei 12, kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwake Usangi kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho, ambapo shughuli hizo zitafanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Kilaweni.

Baada ya hapo, mwili utakabidhiwa kwa familia na kulala nyumbani kwake, kabla ya kufanyika kwa ibada maalum katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mwanga, mnamo Mei 13.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema mwili wa Hayati Msuya unatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) majira ya saa tatu asubuhi ya Mei 12 mwaka huu na kusafirishwa moja kwa moja hadi Wilayani Mwanga.

Aliongeza kuwa wananchi Wilaya ya Hai, Kwasadala, Maili sita, Kiboriloni, Moshi Mjini,YMCA, watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kabla ya shughuli rasmi ya maziko kufanyika kijijini Usangi.

Katika salamu zao za maombolezo, viongozi wa maeneo mbalimbali walimkumbuka Hayati Msuya kama kiongozi mzalendo na mwenye maono.

Diwani wa Kata ya Chomvu, Shaghira Selemani Mchomvu, alisema: “Hayati Msuya alikuwa mstari wa mbele kuhimiza maendeleo ya wananchi, uwajibikaji na kujikwamua kiuchumi. 

Alisema marehemu Msuya aliwahamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi na kuanzisha chombo cha uchumi kwa Wajasiriamali wadogo kiitwacho UWAMWA.

Naye Diwani wa Kata ya Kirongwe, Amiri Sarumbo Mkono, alisema marehemu Cleopa David Msuya, alisisitiza sana elimu kwa watoto na utunzaji wa mazingira, akiongeza kuwa alitekeleza hayo kwa mafanikio makubwa.

Maziko ya Hayati Msuya yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa serikali, vyama vya siasa, taasisi binafsi, viongozi wa dini na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza waombolezaji katika tukio hilo la kitaifa.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.