MWANGA-KILIMANJARO
Watanzania wametakiwa kumuenzi na kuiga tabia njema alizokuwa nazo Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Cleopa David Msuya, aliyefariki dunia Mei 7, 2025, jijini Dar es Salaam, kama heshima kwa mchango wake mkubwa kwa taifa.
Askofu mteule wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Dkt. Daniel Mono, aliyasema hayo Mei 12,2025 wakati wa hafla ya kuaga mwili wa marehemu Mzee Msuya iliyofanyika katika uwanja wa CD Msuya, uliopo Mwanga mjini mkoani Kilimanjaro.
"Mzee Msuya, baada ya kupata elimu yake, alipata nafasi ya kulitumikia taifa na akafanya hivyo kwa uadilifu, uaminifu na ujasiri mkubwa," alisema Dkt. Mono.
Aliongeza kuwa marehemu alikuwa chimbuko la mshikamano, upendo na ushirikiano miongoni mwa Watanzania, na alikuwa mwalimu wa wengi katika masuala mbalimbali ya maisha.
"Mzee Msuya aliishi kwa kuyatenda aliyoyaamini, na hilo ndilo lililokuwa msingi wa kazi na utumishi wake kwa umma, akiwa mbunge na kiongozi serikalini," alifafanua.
Aidha, alieleza kuwa marehemu alimcha Mungu na kumtumikia kwa moyo wa uaminifu bila kujali vyeo mbalimbali alivyowahi kushikilia.
"Watanzania tumshukuru Mungu kwa kutupa Baba huyu wa taifa, aliyewajali watu na kuwahudumia kwa moyo wake wote. Ametuachia alama nyingi za kuigwa," alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema kuwa Mzee Msuya ameacha urithi wa unyenyekevu na busara, ambao unapaswa kudumishwa na vizazi vijavyo.
"Alikuwa mshauri wa karibu wa viongozi wa mkoa, na hakuacha kupigania maendeleo ya wananchi hata baada ya kustaafu na kuachana na siasa," alisema Babu.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda alisema Mzee Msuya atakumbukwa kwa uthubutu wa kusema ukweli, hata katika mazingira magumu, jambo lililomletea heshima kubwa wakati wote wa uhai wake.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi, Wazri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hamza Hassan Juma, Mama Tunu Pinda, Balozi Mstaafu Dkt. Asharose Migiro, pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na mlezi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Rabia Abdallah Hamid.