“MSUYA HAKUWA WA MWANGA PEKEE, ALIKUWA WA TAIFA” – PROF. NDAKIDEMI

USANGI-MWANGA

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, amesema kuwa kifo cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Cleopa David Msuya, ni pigo kubwa si tu kwa wakazi wa Wilaya ya Mwanga, bali kwa Tanzania nzima.

Akizungumza Mei 13, 2025, katika ibada ya mazishi ya Msuya yaliyofanyika kijijini kwake Chomvu, Tarafa ya Usangi, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Prof. Ndakidemi alisema taifa limepoteza mmoja wa viongozi waadilifu na wenye busara ambao walitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

“Licha ya kustaafu kwake, viongozi wengi waliendelea kutafuta ushauri na busara kutoka kwa Mzee Msuya, alikuwa kiongozi mwenye maono, aliyetoa mchango mkubwa kwa taifa na hasa kwa wana Mwanga,” alisema Prof. Ndakidemi.

Cleopa Msuya alifariki dunia Jumatano, Mei 7, 2025, jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo, na alizikwa nyumbani kwake Usangi Mei 13, 2025.

Aidha Mbunge Ndakidemi alieleza kuwa Msuya alikuwa mwasisi wa Wilaya ya Mwanga na alihakikisha maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali yakiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, na mazingira.

“Alikuwa kiongozi bora, mzalendo wa kweli, na mfano wa kuigwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo, alitumia maisha yake kuwatumikia wananchi kwa moyo wa dhati na bidii,” aliongeza.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.