MOSHI-KILIMANMJARO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha maalum la pili la utamaduni la mkoa wa Kilimanjaro, ambapo atamsimika rasmi Frank Marealle kuwa Mwenyekiti wa Machifu wa mkoa huo., tukio hilo litafanyika Mei 20, 2025, katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 5,2025 na Katibu wa Umoja wa Machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Mselle, alisema tamasha hilo litakuwa la kipekee na kihistoria, likihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimila na serikali kutoka maeneo tofauti ya nchi.
“Tamasha hili ni la pili kufanyika mkoani hapa baada ya lile la kwanza Januari 2022, ambapo mgeni rasmi alikuwa Chifu Hangaya. Safari hii tunatarajia heshima ya pekee ya kuwa na Rais Dkt. Samia kama mgeni rasmi na atakuwa na jukumu la kumsimika Marealle kuwa mwenyekiti wetu wa kimkoa,” alisema Mselle wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Moshi.
Alieleza kuwa Frank Marealle ndiye mwanzilishi wa Umoja wa Machifu Tanzania, na baada ya kumaliza muda wake wa uenyekiti kitaifa, machifu wa mkoa wa Kilimanjaro waliona ni busara aendelee kuhudumu katika nafasi ya mwenyekiti wa mkoa.
Alisema kuwa kila mkoa una utaratibu wa kuwa na kiongozi wa kimila, na Frank Marealle ndiye mwanzilishi wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT), baada ya kung’atuka uongozi wa taifa, machifu wa Kilimanjaro waliona ni muhimu aendelee kuwa mwenyekiti wa mkoa.
"Katika tamasha hili pia litahusisha shughuli mbalimbali, zikiwemo utoaji wa tuzo kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ndiye Chifu Mkuu wa Machifu nchini,"alisema Mselle.
Aidha alisema tamasha hilo litatanguliwa na matukio mbalimbali, ikiwemo mkutano mkuu maalum wa Viongozi wa kimila zaidi ya 100 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
"Viongozi hawa wa kimila wanatarajiwa kukutana mkoani hapa Mei 19 mwaka huu katika hoteli ya Marangu kwa ajili ya kushiriki mkutano mkuu maalum wa kuliombea Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka huu".
Alisema mkutano huo ni jukwaa la kuwakutanisha machifu kutoka pande zote za nchi kwa lengo la kufanya maombi maalum kwa ajili ya taifa, pamoja na kupokea mawasilisho kutoka serikalini kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya uongozi wa Awamu ya Sita, ukiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Katika mkutano huu viongozi wa kimila watapokea taarifa juu ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na serikali, sambamba na kujadili changamoto zinazozikabili jamii zetu,” alisema Mselle.
Aliongeza kuwa "Katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye mchakato wa kidemokrasia, maombi na ushiriki wa viongozi wa kimila unatoa mchango wa kipekee katika kuimarisha amani, mshikamano na ustawi wa kitaifa."
Alisema pamoja na agenda ya maombi kwa taifa, mkutano huo utagusia kwa kina masuala ya mmomonyoko wa maadili katika jamii, hasa kwa watoto na vijana, sambamba na ukatili wa kijinsia unaoendelea kushuhudiwa kwenye maeneo mbalimbali.
Alifafanua kwamba mkutano huo ni wa kila mwaka na hutumika kama fursa ya kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto za mwaka uliopita, pamoja na kupanga mikakati ya mwaka unaofuata.
Pia, alisema kuanzia Mei 17, mwaka huu kutakuwa na maonesho ya biashara katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, ambapo siku ya tamasha, Mei 20, kutakuwa na maandamano yatakayoongozwa na Brass Band ya Polisi, yakihusisha wanafunzi wa vyuo vikuu 32 vya mkoa wa Kilimanjaro, walimu wazalendo, baba lishe, mama lishe pamoja na wapanda mlima.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo, Chifu wa Marangu, Frank Marealle, alisema mkutano huo ni jukwaa la viongozi wa kimila kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kitaifa kuhusu maendeleo, maadili, na mwelekeo wa jamii ya Watanzania.
“Wazee wa kimila na machifu wana nafasi kubwa ya kukumbusha jamii juu ya malezi yenye misingi ya maadili. Kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili, na sisi tuna jukumu la kuhakikisha watoto na vijana wanalelewa katika misingi ya mila na desturi njema,” alisema Chifu Marealle.
Aliongeza kuwa tamaduni ni kiini cha malezi bora, na ndiyo msingi wa mshikamano na maendeleo. huku akitoa pongezi kwa serikali ya Awamu ya Sita kwa kutambua mchango wa viongozi wa kimila katika kusimamia na kudumisha utambulisho wa Kitanzania.
“Tunaendelea kutambulika na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ya wajibu wetu katika kulinda na kusimamia misingi ya mila, tamaduni na maadili ya Mtanzania,” alisisitiza Chifu Marealle.
Mkutano huo pia unatarajiwa kutoa dira na maazimio yatakayosaidia si tu kuelekea uchaguzi kwa utulivu, bali pia kujenga jamii yenye maadili, mshikamano na maendeleo endelevu.




%20kutoka%20kulia%20akiwa%20katika%20picha%20ya%20pamoja%20na%20machifu%20kutoka%20wilaya%20za%20mkoa%20wa%20Kilimanjaro%20baada%20ya%20kumalizika%20kwa%20kikao%20cha%20maandalizi%20ya%20mkutano%20mkuu%20maalu%20%20Mei%2019,%20mwaka%20huu.jpg)







%20kutoka%20kulia%20akiwa%20katika%20picha%20ya%20pamoja%20na%20machifu%20kutoka%20wilaya%20za%20mkoa%20wa%20Kilimanjaro%20baada%20ya%20kumalizika%20kwa%20kikao%20cha%20maandalizi%20ya%20mkutano%20mkuu%20maalu%20%20Mei%2019,%20mwaka%20huu.jpg)