MBUNGE NDAKIDEMI AHOJI MKAKATI WA SERIKALI KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA YA INTERNATIONAL SCHOOL- KIBOSHO- KNCU KWA RAFAEL

DODOMA.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, amehoji Bungeni kuhusu hatua za Serikali katika kuhakikisha ujenzi wa barabara ya International School–Kibosho KNCU hadi kwa Rafaeli unakamilika kwa mujibu wa mkataba.

Akiuliza swali la nyongeza katika kikao cha Bunge kilichofanyika Alhamisi Mei 2,2025 Profesa Ndakidemi alisema wananchi wa Tarafa ya Kibosho wamefurahishwa na hatua ya Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii.

"Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha barabara hii inakamilika kama ilivyo kwenye mkataba?" alihoji Profesa Ndakidemi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema tayari mkandarasi wa mradi huo amepatikana na ameshaanza mchakato wa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kilomita sita za barabara hiyo.

Naibu Waziri Kasekenya alisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kikamilifu ili kuboresha huduma za usafiri na kuinua uchumi wa wakazi wa eneo hilo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.