MOSHI-KILIMANJARO.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro limepongezwa kwa juhudi zake za kutoa elimu ya kuzuia majanga ya moto kwa watoto na jamii kwa ujumla.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwereni, iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Moshi Sister Aniseta Madundu, alitoa pongezi hizo Mei 4, 2025 wakati akipokea misaada mbalimbali iliyotolewa na jeshi hilo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Zimamoto Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Mei 4.
Alisema kuwa elimu inayotolewa na Jeshi la Zimamoto imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa usalama dhidi ya moto kwa watoto na wakazi wa maeneo ya karibu.
"Tunawashukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa namna wanavyojitolea kuelimisha jamii hasa watoto wadogo ambao ni kizazi cha leo na kesho, elimu hii ya zimamoto waliyopata watoto hapa shuleni si ya kawaida itawasaidia kuokoa maisha yao,"alisema Sister Aniseta.
Sister Aniseta alisema kuwa elimu inayotolewa na Jeshi hilo imekuwa msaada mkubwa kwa wananfunzi kuelewa namna ya kujikinga na madhara ya moto, pamoja na hatua za kuchukua pindi ajali ya moto inapotokea.
Akikabidhi misaada hiyo kwa uongozi wa shule hiyo Mrakibu Msaidizi wa Jeshi hilo Jeremiah Mkomagi, alisema katika maadhimisho hayo, Jeshi la Zimamoto liligawa misaada ya kijamii na kutoa mafunzo mafupi kuhusu namna ya kukabiliana na majanga ya moto kwa wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema kuwa utoaji wa elimu kwa jamii ni sehemu muhimu ya majukumu yao ya kila siku na kwamba wataendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kinga dhidi ya majanga ya moto.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya uongozi wa shule ya msingi Mwereni Mwalimu wa shule hiyo Clara Ullomi, alilishukuru Jeshi hilo kwa misaada waliyoitoa kwa watoto wenye mahitaji maalumu, huku akisema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka, kwani baadhi ya watoto ni yatima na wengine wanatoka kwenye familia zisizo na uwezo wa kumudu mahitaji yao ya kila siku.
"Tuiombe jamii iendelee kujitokeza kuwasaidia watoto hawa, mahitaji yao ni makubwa na yanahitaji mshikamano kwa wote ili kuwajengea maisha bora,"alisema.
Aidha aliitaka jamii kuwafichua wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu badala ya kuwapeleka shule, akisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maisha ya mtoto na hutoa nafasi sawa kwa kila mmoja.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, mwanafunzi Michael Tarimo na Jaslin Shija, wamelishukuru Jeshi la Zimamoto kwa msaada na elimu waliyopewa, wakisema kuwa wamejifunza mambo muhimu kuhusu usalama wao na namna ya kujikinga dhidi ya moto.
Katika hafla hiyo wanafunzi hao walishiriki katika maonesho ya vitendo vya kuzima moto, walijifunza matumizi ya vifaa vya dharura, na walipata fursa ya kuuliza maswali kutoka kwa maofisa wa zimamoto waliokuwa wakitoa mafunzo hayo.
Maadhimisho Siku ya Zimamoto Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa kuwakumbuka askari wa zimamoto waliopoteza maisha wakiwa kazini, wakiwemo watano waliokufa katika moto wa msitu Jimbo la Victoria, Australia.












