WAZEE WA KITUO CHA NJORO WAPOKEA MSAADA KUTOKA RED CROSS KILIMANJARO

MJI  MPYA

Wazee wasiojiweza wanaolelewa katika Kituo cha Wazee cha Njoro, kilichopo Kata ya Mji Mpya halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamepokea msaada wa kibinadamu kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) Mkoa wa Kilimanjaro, hatua iliyowagusa na kuwapa faraja kubwa.

James Joseph na Catarina Bartazari ni miongoni mwa wazee waliopokea msaada huo na walitoa shukrani zao kwa Red Cross kwa kuwajali na kuwakumbuka, kuja kuwatembelea na kuwapatia misaada hiyo ambapo wamesema kuwa maisha yao yanategemea sana misaada kutoka kwa wadau kama ambavyo wametoa Red Cross.

"Natoa shukrani sana kwa Red Cross kuja kututembelea na kutupatia msaada huu, kwani maisha yetu yanategemea sana misaada kutoka kwa wadau kama ninyi," alisema James Joseph.

Catarina Bartazari naye alisema kwa furaha: “Tunasukuru sana Red Cross kwa kuja kututembelea na kutupatia msaada huu.”

Akikabidhi misaada hiyo Mratibu wa Red Cross Mkoa wa Kilimanjaro, Mohamed Kisima, alisema Red Cross imeguswa na kuwatembelea wazee hao na kuwapatia misaada hiyo kama sehemu ya kuthamini utu wa binadamu, ikiwa ni mojawapo ya kanuni kuu za Red Cross.

"Tumeguswa kuwatembelea wazee wetu na kuwapatia msaada huu kama sehemu ya kuthamini utu wa binadamu, ikiwa ni mojawapo ya kanuni kuu yetu ya Red Cross."

"Misaada tuliyoitoa kwa wazee wetu hawa ni pamoja na mchele, mafuta ya kupikia, sabuni za kuogea na kufulia, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Red Cross itakayofanyika Mei 10 mwaka huu Mkoani Dodoma sambamba na kuadhimisha miaka 63 ya kuzaliwa kwa Red Cross Tanzania.

Naye Diwani wa Kata ya Mji Mpya, Abuu Shayo, aliipongeza Red Cross kwa hatua hiyo na kusisitiza kuwa kusaidia wazee ni ibada yenye baraka kubwa.

"Katika maandiko matakatifu tumeagizwa kuwasaidia wajane, yatima na wasiojiweza, msaada huu unathamani kubwa sana kwa wazee wetu," alisema.

Awali akizungumza mlezi wa kituo hicho, Maria Massawe, alisema kituo cha Njoro kinahudumia wazee 14, kwa usaidizi wa serikali na wadau mbalimbali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alitoa shukrani kwa Red Cross kwa kazi kubwa wanayoifanya katika jamii na kusema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na taasisi binafsi kuwahudumia watu wanaohitaji msaada.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.