WAKAZI WA KATA YA NJORO WAJIUNGA KWA UMOJA KUSAPOTI JUHUDI ZA DIWANI ZUBERI KIDUMO

NJORO.

Wakazi wa Kata ya Njoro Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamejitokeza kwa wingi kwa umoja wao kusaidia juhudi za Diwani wa kata hiyo Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo kwa kupanda ukoka kwenye uwanja wa Railway, kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya Zuberi Cup-2025 yanayotarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka huu.

Mariam Hamisi, mmoja wa akina mama walioshiriki katika kupanda ukoka, alielezea furaha yake kuhusu mradi huo. 

“Kupanda ukoka ni hatua nzuri kwa ajili ya jamii yetu, kukamilika kwa uwanja huu kutanufaisha wengi, ikiwemo akina mama kama sisi, kwa kutoa nafasi ya kufanya biashara wakati wa mashindano, na pia kuhamasisha vijana kushiriki zaidi katika michezo,” alisema Bi. Mariam.

Naye Mwajuma Ally alisema "Ni jambo la furaha kuona akina mama na vijana kujitokeza kwa wingi kusaidia kazi hii muhimu pasipo kulipwa chochote, lengo moja tu ni kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Diwani Zuberi Kidumo, kwani kwa kushirikiana, tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli,"alisema.

Mkazi mwingine Amina Juma  alisema "Kama ilivyo kwa mashindano mengine ya michezo, Zuberi Cup-2025, inatarajiwa kuwa ni chanzo cha kuhamasisha na kuendeleza michezo miongoni mwa vijana, huku ikiwapa nafasi ya kukutana na kushindana kwa njia ya afya na kufurahisha."

Aliongeza kuwa "Diwani Zuberi Kidumo ameonyesha uongozi wa kipekee kwa kuleta greda lililochimba na kusawazisha ardhi ya uwanja wa Railway, jambo ambalo limeongeza matumaini kwa wachezaji na wananchi wa kata hiyo,"alisema Amina.

Akizungumza na waandishi wa habari Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, alisema "Kupanda ukoka huu utasaidia pia kuimarisha ardhi na kupunguza mmomonyoko,” alisema Diwani Zuberi Kidumo.

"Hatua hii inakuja kama sehemu ya mipango yangu ya kuboresha mazingira ya michezo, ikiwa ni pamoja na kufanya uwanja kuwa bora kwa mashindano haya."alisema Mhandisi Kidumo.

Alifafanua kuwa “Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wachezaji wetu wanakuwa na mazingira bora ya kucheza, hivyo tumejizatiti kuandaa uwanja wa Railway ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa".

Kwa upande wake katibu wa Chama cha Soko Moshi (MMFA) Mwl. Japhet Mpande alisema maboreshio ya uwanja huo yameonyesha dhamira ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuboresha mazingira ya michezo kwa vijana na wakazi wake.

Aidha Mwl. Mpande alimshukuru Mstahiki Meya Zuberi Abdallah Kidumo kwa hatua ya kuufanyia marekebisho uwanja wa soka wa Railway, uliopo kata ya Njoro.

"Ujenzi wa uwanja huu kwetu sisi ni manufaa makubwa sana, tutakuwa na ligi daraja la nne, ligi ya mkoa hata mashindano mbalimbali yatakuwa yakifanyika hapa,"alisema.

Mashindano ya Zuberi Cup-2025 yatakuwa ni tukio la kipekee kwa vijana na jamii ya Kata ya Njoro, kwani yatatoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao na kujenga mshikamano miongoni mwao. 

Pia mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya kijamii, ikiwemo kuhamasisha biashara ndogo ndogo na kuongeza shughuli za kijamii katika kata hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.