DIWANI KATA YA KALOLENI AKABIDHI ZAWADI YA SARE KWA VIJANA WA UVCCM



MOSHI.

Diwani wa Kata ya Kaloleni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Nasibu Abdallah Mariki, amekabidhi zawadi ya sare kwa vijana wa hamasa ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wa kata hiyo waliopata kushiriki kambi maalum ya mafunzo mwaka jana.

Mariki ameyasema hayo Aprili 18, 2025 wakati wa hafla fupi ya kukabidhi sare hizo kwa vijana 15 wa UVCCM kata ya kaloleni, kama ishara ya kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa vijana hao katika shughuli za kijamii na kisiasa, hususani katika kuhamasisha maendeleo ya kata ya Kaloleni.

Alisema kuwa sare hizo zina thamani ya Shilingi 485,000 na kwamba si mara yake ya kwanza kuonyesha kuthamini vijana kwani hata mwaka jana aliwazawadia sare Wajumbe wa Baraza la UVCCM ngazi ya kata.

"Sare hizi ni sehemu ya vitendea kazi vya jeshi la vijana, nimeona ni vyema kuwashonea sare ili wawe tayari kwa mapambano yajao,"alisema.

Katika hotuba yake hiyo Mariki aliwaasa viongozi wenzake kuacha kuwatumia vijana kisiasa kisha kuwatupa, huku akitoa mfano wa mti wa "Mambo" unaotumika kuchomea nyama.

"Niwaombe Vijana msikubali kutumika kama mti wa 'Mambo' kule Umasaini,  mti wa mambo unaotumika kuchoma nyama baada ya kazi kuisha kisha hutupwa, nawaombeni sana tuwathamini, tuwajenge na tuwaandae kwa majukumu ya taifa."alisema Diwani Mariki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Kaloleni Mohamed Mweisange alimpongeza Diwani Mariki kwa moyo wake wa kupata na kugawana na vijana.

"Diwani  Mariki amekuwa ni mtu wa kuwatia moyo na kuwasaidia kila mara tunapomhitaji, hakuna hata siku moja jambo la UVCCM lililowahi kufikishwa kwake na kulikataa,"alisema Mweisange.

Aidha alisema ushirikiano huo umeongeza morali kwa vijana wa kata hiyo na kuwajengea ari ya kuendelea kujitoa katika shughuli za kijamii na kisiasa.

Nao baadhi ya vijana wa UVCCM  walioopokea sare hizo Zahoro Mipango, Mwajuma Selemani, Amina Juma na Mariamu Ally, walimpongeza, Diwani Mariki kwa moyo wake wa kuthamini juhudi zao na kuahidi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na maendeleo ya kata.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.