MOSHI-KILIMANJARO
Muu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Calvin Koola, ametoa wito kwa Wakristo nchini kuhakikisha wanamshirikisha Mungu kwa kumkabidhi mafanikio yao, hususan wanapojenga au kununua nyumba, kabla ya kuanza kuishi ndani yake.
Akihubiri katika ibada maalumu ya uzinduzi wa kubariki nyumba ya mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Frank Marealle, Mchg. Calvin Koola, amehimiza umuhimu wa kuiombea na kuikabidhi nyumba kwa Mungu kabla ya kuhamia rasmi, kama ishara ya shukrani na kujenga msingi wa Kiroho ndani ya familia, ambapo hafla ya uzinduzi wa kubariki nyumba hiyo ilifanyika kijiji cha Msae Kinyambuo, kata ya Mwika Kaskazini wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema baraka zinazopatikana iwe ni nyumba, mume, mke, gari au watoto zinatoka kwa Mungu, lakini wako baadhi ya waumini wanapopata mafanikio hayo husahau kurudi madhabahuni pa Bwana kumshukuru Mungu.
Alisema kuwa si jambo la Kiroho wala la busara kuhamia kwenye nyumba mpya kabla ya kuikabidhi kwa Mungu, kupitia sala na maombi kwa kuwa nyumba hiyo inakuwa sehemu ya maisha na ulinzi wa familia.
Aidha amesema kuwa mafanikio ya kimwili yanapaswa kuambatana na ukuaji wa kiroho kwa kumshirikisha Mungu katika kila hatua ya maisha, huku akimpongeza Chifu Marealle kwa kufanikiwa kujenga nyumba yake hiyo na kabla ya kuhamia akaoni ni vyema iweze kupata baraka za maombezi kutoka kwa Mungu.
Akizungumza kwa niaba ya Mume wake Chifu Frank Marealle, Rose Marealle, amesema walimuomba Mungu kwa muda mrefu awape uwezo wa kujenga nyumba ya kuishi na familia yake na leo hii wanashuhudia Mchungaji Koola akija kuibariki rasmi kabla hawajahamia, kwani hiyo ni heshima na baraka kubwa kwa familia yake.
Uzinduzi wa nyumba hiyo ulihudhuriwa na waumini wa KKKT, majirani na viongozi wa kijiji, ambapo sala, nyimbo na maombi yaliongozwa kwa nia ya kuiweka nyumba hiyo mikononi mwa Mungu.