Wananchi Kilimanjaro Wakoshwa na Huduma za Ushauri wa Kisheria zinazotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali


MOSHI-KILIMANJARO.

Wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wamejitokeza kwa wingi kupata huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano na Kamati ya ushauri wa kisheria ya mkoa wa Kilimanjaro.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi walifika katika kliniki ya ushari wa kisheria bila malipo wameshukuru na kupongeza hatua ya kusogeza kliniki ya msaada wa kisheria kwani imekuwa msaada mkubwa kwao hasa kwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za wanasheria.

Akizungumza mara baada ya kupata huduma kwenye kliniki ya sheria bila malipo, Mkazi wa Kata ya Mnadani halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani humo Mohamed Marandu, alisema ameridhishwa na huduma hiyo pamoja na maelezo aliyoyapata kutoka kwa Mawakili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku akiamini Kliniki hiyo itawasaidia wananchi wengi kupata haki zao.

“Kupitia kliniki hii nimeweza kupata maelezo mazuri kuhusiana na suala langu la ardhi, Mawakili wamenipokea vizuri na kunieleza hatua sahihi za kufanya ili niweze kupata haki yangu, nawashukuru sana kwa kuja na kutoa elimu hii,”alisema Marandu.

Kwa upande wake mkazi wa Kata ya Shirimatunda  Manispaa ya Moshi Emiliana Maliwa; aliishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendesha kliniki hiyo ya kisheria bila malipo kwa wananchi kwani Ofisi hiyo imezingatia watu ambao hawana uwezo wa kuwalipa wanasheria katika kuwasimamia masuala yao ya kisheria ili waweze kunufaika na huduma hiyo.

“Niwapongeze na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta kliniki hii hapa, ambayo inatolewa bure itatusaidia kwakua inatolewa bila malipo yoyote na naamini wengi tutanufaika sana na huduma hii,”alisema Emiliana 

Mkazi mwingine wa Kata ya Hedaru Isack Ngupa, aliyefika katika kliniki hiyo aliiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya kliniki hiyo mara kwa mara na kupeleka huduma hizo za ushauri wa kisheria katika maeneo ya Vijijini ambako wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya kisheria hivyo kupelekea kupoteza haki zao.

“Niwaombe Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzunguka vijijini kutoa elimu hii, huko kuna changamoto nyingi za kisheria wananchi hawana uelewa wa namna ya kuzitatua, pia watoe huduma hizi mara kwa mara kwani itasaidia sana kupunguza migogoro inayojitokeza katika jamii”.alisema Ngupa.

Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hiyo Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Joseph Shoo, alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi na wengine wametoka katika maeneo ya mbali kuja kupata huduma  zinazotolewa katika Kliniki ya ushauri wa kisheria bila malipo.

“Mwitikio wa wananchi kujitokeza katika kliniki hii ni mzuri, tumeweza kupokea malalamiko mengi yanayohusu masuala ya ardhi, mirathi, jinai, ndoa na masuala ya kijinsia,  baadhi ya malalamiko tuliyo yasikiliza tumeyatatua hapa hapa na mengine tumeyachukua kwa hatua zaidi.”alisema Wakili Shoo huku akiwaomba wananchi wa mkoani humo, kuendelea kujitokeza kwa wingi ili waweze kuhudumiwa.

Kliniki ya sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro ilianza Januari 21 na inaendelea hadi  Januari 27, mwaka huu Katika viwanja vya Stand kuu ya mabasi Moshi.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.