Kampuni ya Magic Builder's International yatoa ufadhili kwa wanafunzi 2,000, yaanza na watoto 150 wa mafundi Rangi na Ujenzi mkoani Kilimanjaro

MOSHI-KILIMANJARO

Kampuni ya Magic Builder's International, inatarajia kuwafaadhili takribani wanafunzi 2,000 wanaosoma shule za msingi za serikali kwa kuwalipia mahitaji mbalimbali ya shule ikiwemo fedha kwa ajili ya chakula, nguo za shule, madaftari na kalamu ili watoto waweze kusoma kwa amani.

Hayo yamesemwa Januari 22,2025 na Mkurugenzi wa Magic Builder's International  David Barongo, wakati wa hafla ya kutoa ufadhili kwa wanafunzi 150 ambao ni watoto wa mafundi rangi na ujenzi mkoani Kilimanjaro.

Barongo alisema katika kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu Serikali ilitangaza sera ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita; hata hivyo kuna michango mingine ambayo mzazi wazazi anatakiwa kuichangia ili watoto waweze kusoma kwa amani.

“Michango hii ina baraka za Serikali kwa vile wazazi na walezi hushirikishwa na wakiridhia kuwa inaidhinishwa na Mkuu wa Wilaya husika; ni vyema tukungana Serikali ili watoto wetu wapate elimu ambayo ni muhimu kwa ajili  ya maisha yao ya baadaye”, alisema Barongo.

Akizungumzia mchango wa Kampuni ya Magic Builders International Limited kwa wanafunzi, Barongo alisema kampuni hiyo imeamua kurudisha kwenye jamii CSR kwa kile wanachokipata kupitia shughuli zake ambazo zinahusiana na mauzo ya bidhaa za ujenzi.

“Wateja wetu wakubwa ni mafundi ujenzi pamoja na wananchi wengine hivyo michango yetu hii imewalenga wanafunzi ambao ni watoto wa Watanzania wenzetu ambao nao wanatoa michango yao kupitia manunuzi ya bidhaa zetu na hivyo kuifanya kampuni ya Magic Builders International Limited, iendelee kuweko na pia kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali.”alisema.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema mchango huo umelenga kuunga mkono juhudi za Serikali za Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan zinazolenga kuimarisha sekta ya elimu.

“Leo Kampuni ya Magic Builders International Limited, tutawakabidhi Sh milioni 7.5 ambazo zitawawezesha wazazi na walezi kuchangia kwa ajili ya chakula shuleni ili kuondoa mazingira magumu kwa watoto wao wawapo shuleni ili waweze kuwa  na utulivu wakati wa masomo yao darasani,”alisema Barongo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha mafundi Rangi na Ujenzi mkoa wa Kilimanjaro (CHAMARUKI) Michael Kimea, aliishukuru Kampuni ya Magic Builders International kwa kuwakumbuka wanafunzi haswa katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wanarudi mashuleni na  wengine ndiyo kwanza wanaanza elimu ya msingi.

Awali akizungumza Katibu  mtendaji wa CHAMARUKI mkoa wa Kilimanjaro Casmiry John Toto, alisema kuwa mchango huo utachangia wanafunzi, wazazi pamoja na walezi wao kutimiza ndoto zao za kuhakikisha watoto wanapata elimu nzuri.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.