Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya watu walio na magonjwa ya
maambukizi ukiwemo ule wa Kifua Kikuu, wanapata changamoto ya afya ya akili.
Changamoto hiyo inasababishwa na sonona ambayo inasababishwa na mawazo
mengi wanayokuwa nayo wagonjwa hao kutokana na kuugua kwa muda mrefu.
Hayo yameelezwa na Daktari Bingwa wa Magonwja ya Akili kutoka hospitali ya
Taifa Muhimbili Saidi Kuganda wakati wa semina ya siku nne, kwa ajili ya
madaktari na wauguzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi
Kibong’oto (KIDH) iliyofanyika Siha, mkoani Kilimanjaro.
“Watu wengi wakipata maradhi ambukizi haswa yale yanayochukua muda mrefu,
hujikuta wakiwa na mawazo mengi kutokana na kuwa na maradhi hayo na kuwafanya
waache shughuli zao, hili huwasababishia kuwa na msongo wa mawazo na hatimae
kujikuta wakiingia kwenye changamoto ya afya ya akili”, alisema.
Akizungumzia tahadhari ambayo watu wanahitaji kuchukua ili kuepuka
changamoto ya maradhi ambayo husababisha afya ya akili, Dk. Kuganda alisema
hawanabudi kuepuka tabia ya kutumia dawa za kulevya.
“Matumizi ya dawa za kulevya haswa yale ya kutumia sindano ambazo hujichoma
wahusika husababisha kuchangia maambukizi ya maradhi ambayo hatimae hupelekea mtu
kuwa na changamoto ya afya ya akili hapo baadaye”, alisema na kuongeza, watu
hawana budi kujiepuesha na mitindo ya maisha kama vile matumizi ya dawa za
kulevya ambayo yanaweza kuharibu maisha yao ya baadaye.” Dk. Kuganda.
Akifugua semina hiyo, Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa
Ambukizi Kibong’oto (KIDH) Dk. Leonard Subi amesema semina hiyo inalenga
kuwaelimisha watoa huduma za afya hospitalini hapo kuhusu jinsi ya kutambua na
kuwuhudumia wagonwja wenye chanagmoto ya akili haswa wale wanaougua muda mrefu.
“Wawezeshaji katika semina hii wametoka MUHAS na Chuo kikuu cha
Kikatoliki Mwenge (MWECAU) ambapo watawajengea wataalam wetu hapa KIDH uwezo na namna bora ya kuwahudumia wagonjwa wetu,
ambao huwa tunakaa nao kwa muda mrefu”, alisema Dk. Subi.
Aliongeza, “Kama mnavyofahamu
wagonjwa katika hospitali yetu ya Kibong’oto wanatoka maeneo mbalimbali na
matibabu yao ni ya muda mrefu, hivyo ni vyema wataalam wetu wakapata elimu ya ziada
ya jinsi ya kuwahudumia haswa ikitiliwa maanani wanakaa na wagonjwa hao kwa muda
mrefu sana”.
Aidha Dk. Subi
aliwashukuru wafadhili kutoka LHL International kutoka nchini Norway, ambao
wamefadhili semina hiyo sambamba na kufadhili matibabu ya wagonjwa wanaopata
huduma zao hospitalini hapo kwa mdua mrefu.
“Wafadhili hawa pamoja
na Serikali wamekuwa wakitoa msaada mkubwa katika kutoa huduma za chakula,
nguo, dawa pamoja elimu ambayo KIDH hutoa maeneo mbalimbali hapa nchini kuhusu
jinsi ya kujikinga na maambukizi ya kifua kikuu”, alisema Dk. Subi.
Kwa upande wa mtaalam
wa afya ya akili (Mwanasaikolojia) kutoka Chuo cha Kikatoliki Mwenge Godfrey
Mbowe, amesema warsha hiyo, imelenga kuwawezesha watoa huduma za afya,
madaktari na wauguzi kujua vionjo vya kiseikolojia vitakavyo wasaidia jinsi ya
kushughulika na wagonjwa.
Naye mtaalam wa huduma
za kisaikolojia (Psychological Care) kutoka hospitali maalum ya Taifa ya
Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Leocadia Tito Mtweve amesema, mafunzo hayo
yamewahusisha wauguzi wanatoa huduma kwa wagonjwa wa TB Sugu (MDR).
“Tumeona ni vizuri
watumishi hawa ambao ni madaktari na wauguzi wanaotoa huduma kwa wagonjwa Kifua
Kikuu wapate elimu inayohusiana na afya ya akili kwani wanakaa na wagonjwa hawa
kwa mrefu hivyo wanapitia changamoto mbalimbali,” alisema Mtweve.
Afisa Ustawi wa Jamii
KIDH Wazoel Yohana Mshana, Amesema mafunzo ya afya ya akili, kwetu sisi
yatakuwa na tija, kwani kwa kipindi kirefu tumekuwa tukiwahudumia wagonjwa
wa TB Sugu, wanaotoka katika mikoa tofauti hapa nchini ambao wanakuja na
tamaduni zao tofauti.
“Kupitia mafunzo haya
ambayo yameratibiwa na taasisi ya LHL International, kwetu sisi wafanyakazi
yatatusaidia namna ya kupambana na magonjwa haya ya afya ya akili kwani
yamekuwa yakitupa wakati mgumu katika kuhudumia wagonwja wenye changamoto hizo”,
alisema.Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH) Dk. Leonard Subi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Warsha ya siku Nne ya kuwajengea uwezo Madaktari na Wauguzi wanaowahudumia wagonjwa wa Kifua Kikuu ambao wana kaa kwa muda mrefu hospitalini.
Dk. Leonard Subi (kushoto) Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto akisalimiana na Daktari Bingwa wa Magonwja ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Saidi Kuganda.
Daktari Bingwa wa Magonwja ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Saidi Kuganda
Mtaalam wa Afya ya Akili (Mwanasaikolojia) kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge Godfrey Mbowe (MWECAU).