MOSHI-KILIMANJARO
Kuanza kutumika kwa Bima ya Afya kwa Wote, kutasaidia kupunguza gharama za matibabu ya Kibingwa yakiwemo
magonjwa ya moyo na hivyo kuwaondolea wananchi mzigo mkubwa wa kulipia gharama
za matibabu.
Hayo yamesemwa Desemba
4,2024 na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, wakati wa ufunguzi wa Kambi
ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Dk. Samia Suluhu Hassan Kanda ya
Kaskazini, walioweka kambi ya siku Tano kuanzia Desemba 2 hadi Sita katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa
Mawenzi.
Akizungumza na wagonjwa
waliofika kutibiwa hospitalini hapo, Babu amesema gharama za
matibabu ya Kibingwa ni kubwa na Serikali imekuwa na jukumu kubwa la kulipia
gharama hizo za matibabu kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kulipia, hivyo kuanza kutumika
kwa Bima ya Afya kwa wote, kutasaidia Wananchi kupata huduma popote walipo hata
kama hawatakuwa na fedha mfukoni katika kipindi
ambacho wataugua.
“Niwaombe sana Bima ya Afya kwa Wote, itakapoanza kutumika, mjiunge kwani itasaidia kupata matibabu mahali popote
pale mlipo na itasaidia kufuatilia matibabu ya mgonjwa kutoka hospitali yoyote
nchini.”amesema Babu.
Aidha mkuu huyo wa mkoa, amewashukuru Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bombo-Tanga, Maunt Meru Jijini
Arusha, Manyara, Hospitali ya Rufaa ya mkoa Mawenzi, KCMC, Benjamini Mkapa na Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong'oto (KIDH), kwa
kukubali kuja kutoa huduma katika mkoa huo.
Pia amesema kuwa, katika kuboresha huduma za afya nchini, mkoa wa Kilimanjaro, umekwisha kupokea kiasi cha Sh bilioni 129, fedha ambazo zimetumika kujenga hospitali mpya wilaya ya Same, Mwanga, Moshi Vijijini na Manispaa ya Moshi, huku Wilaya ya Hai, ikipokea fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na ukarabati wa miundombinu.
Kwa upande wake Katibu
Tawala wa mkoa wa Kilimanjaro KiseoYusufu Nzowa, amesema mwanadamu anapopungukiwa na
rasilimali ya afya utu wake, thamani yake, ubora wake unapungua kwa kiasi
kikubwa na katika kulitambua hilo, Serikali imeamua kufanya maboresho makubwa
kwenye sekta ya afya kwa lengo la kuwawezesha wananchi wake waweze kuwa na afya bora wakati
wote.
“Natamani wananchi wafike
kwa wingi mahali ambapo huduma hizi zinatolewa na wataalam wa afya, kwani Rais Samia Suluhu Hassan, anawajali wananchi wake, ndiyo maana amesogeza
huduma hii karibu na maeneo yenu baada ya kuona changamoto wanazokutana nazo,”amesema Nzowa.
Awali akizungumza Mganga Mfawidhi
wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi Dk. Edina-Joy- Munisi, amesema jumla ya
wagonjwa 1,328 wameweza kuwaona na kati yao wagonjwa 22 wamefanyiwa upasuaji.
Baadhi ya wagonjwa waliofika kutibiwa katika hospitali hiyo, Mary Andrea Mbowe, Aisha Amiri Kidusho, wameshukuru kwa huduma za matibabu walizozipata kutoka kwa timu ya madaktari bingwa na bingwa bobezi wanazozitoa na kusema kuwa kwa kiwango kikubwa wamesaidia kuokoa maisha yao na ya watoto wao.
















