Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri
Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo, amekabidhi hundi ya Sh milioni 2.3 kwa Chama
cha Ushirika na Mikopo cha Bajaj na Bodaboda mkoani Kilimanjaro
(KIBABOT-SACCOS) ikiwa ni gawio la asilimia 20 ya makusanyo ya Sh milioni 12
baada ya kutoa leseni 556.
Aidha Suluo ameipongeza Serikali mkoani Kilimanjaro
kwa kuboresha mazingira ya biashara mkoani humo ambayo yamesaidia kila mmoja
kuchangia Uchumi wa taifa.
Suluo aliyasema hayo Septemba 3, 2024 wakati wa
hafla ya kukabidhi cheti cha Uwakala wa kutoa leseni za LATRA kwa Chama cha
Ushirika na Mikopo cha Bajaj na Bodaboda mkoani Kilimanjaro (KIBABOT-SACCOS)
hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha kuanzia
Mei 2024 hadi Agosti 31 mwaka huu chama hicho kimetoa leseni 556 na kukusanya
zaidi ya Sh milioni 12, hivyo LATRA imewaongezea jukumu la kutoa leseni kwa
magari ya kukodisha zikiwemo Taix.
“Kwa kipindi cha kuanzia mwezi Mei hadi Agosti 31
mwaka huu, wenzetu wa KIBABOT-SACCOS wametoa leseni 556, katika leseni hizi
wameweza kukusanya jumla ya Sh milioni 12,236, 000 na hivyo kuweza kupata gawio
la Sh milioni 2,446,400.” Amesema CPA Suluo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa
Kilimanjaro, Katibu Tawala wa Mkoa Kiseo Yusuf Nzowa, amesema mkoa huo
utaendelea kutoa ushirikiano kwa vijana hao ili kuendelea kukuza Uchumi wao
huku akiwasifu kwa kuwa mkoa wa kwanza kuja na ushirika wa aina hiyo nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya chama hicho cha Ushirika Amani Bendera, ameipongeza serikali kwa kuwaunga mkono vijana akiahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii na kuwa mfano kwa vijana wote nchini.




