Kwaya ya Furahini Majengo, yafanya matendo ya huruma kwa kutoa misaada kwa jamii kuelekea Jubilee ya miaka 50

Waimbaji wa Furahini Choir Majengo Moshi, Katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, wameendelea kufanya matendo ya huruma kwa kutoa misaada mbalimbali ya kijamii kuelekea maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 toka kuanzishwa kwa kwaya hiyo.

Mwenyekiti wa Kwaya hiyo Bi. Joyce Ndossi, ameyqsema hayo  Agosti  4,2024 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea Jubilee ya miaka 50 ambayo kilele chake kitahitimishwa Septemba mosi mwaka huu.

Amesema kwaya ya Furahini, imefanya matendo ya huruma kwa kutoa misaada mbalimbali vikiwemo viti vya kukalia waumini wa Kanisa la KKKT Magadini lililoko Simanjiro mkoani Manyara.

Ndossi amesema, katika kutambua changamoto zinazowakabili watu wenye uhitaji kutoka makundi maalumu, pia wametoa chakula katika kambi ya wazee Njoro, ikiwa ni moja ya njia ya kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuwaimarisha katika kueneza injili kwa njia ya uimbaji.

Kwa upande wake Mwalimu wa Kwaya hiyo Neneka Safiel, amesema Mwenyezi Mungu amegawa vipawa kwa kila mmoja na kuwaomba vijana, kujitoa kwa nguvu zote kwa ajili ya kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti , baadhi ya wazee ambao ndio waanzilishi wa kwanya hiyo, Isaria Kimaro, Nipanema Makane, Tulo Chupa, Christian Materu, na Latness Kaale, wamesema, kumtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji kumekuwa baraka kwao.

Caroline Lema ni miongoni mwa wanakwaya wa mwanzo kujiunga na kwaya hiyo mwaka 1973, amesema  ari ya kumtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji ilikuja baada ya yeye kuugua kwa kipindi kirefu na hatimaye mwenyezi Mungu akamponyesha na ugonjwa uliokuwa ukimsumbua na toka mwaka huo ameendelea kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji hadi sasa.

Naye mlezi wa kwaya ya Furahini ambaye pia ni Mama mchungaji wa kanisa hilo Dorcus Kimaro, ametoa wito kwa vijana kujiunga na kwaya hiyo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.