NGIJINI-MWANGA-KILIMANJARO
Baadhi ya Walimu wanaofundisha shule za msingi Kisangara Juu, Changaravo na Kituvoni, zilizoko Kata ya Ngujini, Halmashauri ya Mwanga, wamelalamikiwa na wananchi kulewa pombe kupita kiasi nyakati za kazi na kisha kwenda darasani kuwafundisha wanafunzi wakiwa wamelewa.
Hayo yalijiri kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, uliofanyika katika Ofisi ya Serikali ya kijiji cha Ngujini kwa ajili ya kupokea kero zinazowakabili wakazi wa kijiji hicho.
Akiwasilisha kero hiyo kwa Mbunge, mkazi wa kijiji cha Ngujini Beatha Daudi, amesema wako baadhi ya walimu wa shule ya msingi Kisangara Juu, Changaravo na Kituvoni zilizopo ndani ya kata hiyo, kulewa pombe nyakati za kazi na kwenda kuwafundisha wanafunzi darasani.
Amesema kero hiyo imekuwa ya kipindi kirefu ya walimu kulewa pombe kupita kiasi wakati wa kazi na kuiomba Serikali kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.
Aidha ameiomba serikali kuwaagiza Waratibu Elimu ngazi ya Kata, kupita kila shule kama ilivyokuwa zamani ili kukagua maendeleo ya walimu hao kwani kero hiyo imekuwa ya muda mrefu jambo ambalo linasababisha ufaulu wa wanafunzi kushuka.
Naye Mkazi wa Ngujini Novatus Mriva, ameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa walimu katika shule hizo, pamoja na walimu wa jinsia ya kike kwenye shule ya msingi Kisangara Juu, yenye walimu wa kiume pekee.
Akijibu kero zilizowasilishwa na wananchi hao, Afisa Elimu Divisheni ya Elimu msingi Jeremia Majoh, amekiri kupokea kero iliyowasilishwa na wananchi hao ya walimu kulewa, ambapo amesema kwamba ataiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, ili kuona uwezekanao wa kupeleka Wataalam wa Seikolojia ambao watawapatia semina ya madhara ya kilevi.
Aidha Kuhusu upungufu wa walimu, afisa elimu huyo amesema Halmashauri ya Mwanga ina jumla ya shule za msingi 110, ambapo waliopo ni 627 huku upungufu ni walimu 371.
Vilevile amewaeleza wananchi hao kufanya msawazo wa walimu ndani ya kata hiyo, ambapo mwalimu mmoja wa kike kutoka shule ya msingi Songoa, watampekela shule ya msingi Kisangara Juu, ili kwenda kuongezaa nguvu katika shule ya msingi Kisangara Juu.




