Manispaa ya Moshi yafunga taa za barabarani zenye thamani ya Sh Ml.12 kuondoa adha ya kutembea giza nyakati za usiku

MOSHI, KILIMANJARO

TAA za barabarani zenye thamani ya Milioni 12 zimewekwa maeneo mbalimbali ya Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro na kuondoa adha ya kutembea nyakati za usiku kwa wakazi na wageni wanaotemelea mji huo.

Hayo yameelezwa mnamo Julai 16, 2024 na Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo,  wakati akizungumzia mafanaikio yaliyopatikana katika jimbo hilo kwa miaka mitatu iliyopita. 

“Mafanikio haya yamepatikana kutokana na fedha ambazo Serikali  Kuu imetoa na inaendelea kutoa kwa ajili ya shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro ikiwemo katika jimbo letu la Moshi Mjini”, alisema.

Alisema yeye kama Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini anaungana na viongozi wa Serikali kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo hilo ambapo kwa mahesabu yale yaliyofanyika jimboni humo ni mengi ikilinganishwa na yale yaliyofanyika takribani miaka 25 iliyopita wakati jimbo likiongozwa na upinzani.

Alisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya uwakilishi mzuri ambao wananchi wa jimbo la Moshi Mjini wanao kwa sasa pamoja na ushirikiano na viongozi wengine wa serikali walioko mkoani humo kwa ujumla.

Akielezea mafanikio mengine ambayo yameshapatikana na yanayoendelea kupatikana katika jimbo hilo, Tarimo alisema ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya Wilaya.

“Serikali imetenga jumla ya Sh Bilioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya Kata ya Ng’ambo; ujenzi wa hospitali hii utakuwa ni wa ghorofa kutokana na uhaba wa ardhi ulioko Halmashauri ya Manispaa ya Moshi”, alisema.

Aliongeza, “Ujenzi huu ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kujenga hospitali za Wilaya nchini kote ambapo mahitaji ni eneo la ukubwa wa kati ya ekari 20 na 50, lakini kwa vile sisi tuna uhaba wa ardhi ujenzi wa hospitali ya Wilaya utakuwa ni wa ghorofa”.

Mbunge Tarimo aliendelea kusema kuwa Serikali pia imetoa zaidi ya Sh Bilioni 12 kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa Moshi ambapo alisema kukamilika kwa ukarabati huo kutachochea kukua kwa uchumi wa Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla kupitia sekta ya utalii.

“Mimi kwa ushirikiano na viongozi wengine mkoani hapa tumepigania ukarabati huu kutokana na ukweli kwamba uwanja huu ni chachu ya kukuza uchumi wa Wilaya na Mkoa wa Kilimanjaro kiuchumi”, alisema.

Katika hatua nyingine Tarimo alitoa rai kwa wananchi wa Jimbo hilo kuungana katika shughuli za Kimaendeleo, badala ya kulumbana ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii.

“Kumekuwa na tabia ya watu kuchafuana katika mitandao ya kijamii, hata mimi ni mhanga wa hali hii; hata hivyo mimi sina muda wa kujibizana na mtu au watu badala yake nitaendelea na shughuli za kuwatumikia watu wa jimbo langu tu”, alisema na kuongeza, kazi waliyonipa ni kushirikiana nao katika kuleta maendeleo na si malumbano ya kisiasa.

“Niwaombe tushikamane muda ukifika tutapimana tu, tutapimana kwa uzito tuone mwenye kilo nyingi tutapimana kwa uwezo wa akili, ufahamu, elimu, maadili na hata umahiri wake katika kuwahudumia wananchi”, alisema Tarimo.

Aidha alitoa rai kwa wananchi wa Jimbo hilo kuhakikisha wanajitayarisha vyema kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijijini na Vitongoji,  unaotarajiwa kufanyiak baadaye mwaka huu.

“Ili kupata ushindi ni vyema tukajitokeza wote kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na kwa wale ambao tayari walishajiandikisha waende kuhakiki taarifa zao; asilimia 50 ya ushindi unatokana na kujiandikisha sambamba na kuwa na mgombea anayekubalika ndani ya jamii”, alisema.

Akizungumza Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdalahh Kidumo, alisema mradi wa taa za barabarani,  utachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika mji wa Moshi, kwani utawawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao hadi nyakati za usiku kwa uhuru na usalama.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake zinazolenga kuboresha upatikanaji  matumizi ya nishati ya umeme Mijini na Vijijini.”alisema Mstahiki Meya Kidumo.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.