MAWENZI, MOSHI
Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya kwa ajili ya Kitengo cha huduma za upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi (MRRH) iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo, ameyasema hayo Julai 15,2024, wakati wa uzinduzi wa gari jipya la Wagonjwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, hafla iliyoenda sanjari na uzinduzi wa Wodi ya upasuaji ya Wanaume iliyopo katika taasisi hiyo.
Amesema ujenzi huo ni mwendelezo wa maboresho ya Sekta ya afya yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita hapa nchini, ikijumuisha mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo la kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.
Aidha Mbunge huyo ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi kwa kusimamia vyema miradi yote, ambapo amesema matokeo ya usimamizi mzuri wa miradi hiyo ni ubora wa majengo yaliyokarabatiwa pamoja na miundombinu mipya iliyojengwa katika hospitali hiyo.
Kaimu Mkuu wa Kurugenzi ya Upasuaji ya MRRH Dkt. Zawadi Mahumbuga amesema kuwa wodi ya upasuaji yenye uwezo wa vitanda 22 ya Wanaume iliyozinduliwa na Mbunge huyo, itasaidia kupunguza changamoto ya uhifadhi wa wagonjwa wanaotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Amesema wagonjwa wanaowapokea ospitalini hapo ni 60 kwa kila mwezi, ambao wanahitaji matibabu ya upasuaji, huku wengi wao ni wale wanaopata ajali; na wodi hiyo mpya itasaidia kupunguza changamoto ya ongezeko la idadi ya watu.
Naye Afisa Muuguzi kiongozi Idara ya Upasuaji kitengo cha Wanaume Sofia Minja, amesema wanakabiliwa na upungufu wa wauguzi katika kitengo hicho ukilinganisha na idadi ya wagonjwa wanaowapokea na kuiomba Serikali kuwaongezea idadi ya wauguzi ili waweze kutoa hduma kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) Dkt. Edna-Joy Munisi, amesema Serikali imetenga na inaendelea kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi unaoendelea wa jengo litakalotumika kwa huduma za afya ya dialysis.






