Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka
DUTCH CORNER, SANYA JUU
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro Dkt. Christopher Timbuka, amesema Serikali Wilayani humo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukuza Sekta ya Utalii kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Wilayani humo.
Dkt. Timbuka ameyasema hayo jana wakati akizindua tamasha la michezo la West Tour Kili Marathon kwa mwaka wa 2024, lililofanyika eneo la Shamba la Miti West lililoko Wilayani humo.
“Sekta ya utalii inaendelea kukua kwa kasi kubwa hapa nchini na Wilaya yetu ni moja wapo ya maeneo ya nchi yetu ambako kuna vivutio vingi vya utalii, hivyo tunawakaribisha na tuko tayari kushirikiana na wadau wa utalii kuvitanngaza vivutio hivi na hata kuwa hudumia watalii watakofika toka ndani na nje yetu”, amesema Dkt. Timbuka.
Ameongeza, “Serikali inaendelea na michakato mbalimbali inayolenga kukuza sekta ya utalii hapa nchini; hivyo tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kukuza utalii wa nchi yetu tena kwa vitendo, kwetu sisi ni kuunga mkono juhudi zake na zile za serikali kwa ujumla ili malengo ya kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea nchi yetu izidi kuongezeka”, amesema.
Akizungumzia tamasha hilo Mkuu huyo wa Wilaya , amesema kuwa uweko wake (Tamasha la West Kili Tour Challenge 2024) ni moja wapo ya hatua kubwa za kukuza utalii wilayani humo, kazi ambayo amesema itafanywa vyema na washiriki wanaofika wilayani humo kila mwaka.
“Washiriki wa tamasha hili ambalo hufanyika kila mwaka ni mabalozi wazuri wa kuvitangaza vivutio vilivyoko kwenye wilaya yetu, haswa ikitiliwa maanani tamasha hili pia linashirikisha watu kutoka nje ya nchi”, amesema.
“Sisi kama Serikali tunawapongeza sana waandaji wa mashindano haya ya utalii; mojawapo ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi, kuanzia kipato cha mtu mmoja mmoja; tamasha hili linatimiza malengo haya”, amesema DC Timbuka.
Akiongea katika hafla hiyo, Msaidizi wa Meneja wa Shamba la Miti West Kilimanjaro Mhifadhi Godfrey Baraka amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha wananchi kutumia fursa za kitalii zilizoko wilayani humo kwa ili kuinua vipato vyao na uchumi wa wilaya kwa ujumla.
“Kwa muda wote wa miaka misimu minne ya tamasha hili, uwekezaji umekuwa ukiongezeka, sambamba na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja”, amesema Mhifadhi Baraka.
Ameongeza, “Pia washiriki wanapata fursa ya kufahamiana, kubadilishana mawazo na pia kupeana ushauri unaohusiana na kukuza biashara hususani zinazohusiana na sekta ya utalii; hili limesaidia wadau wengi wa utalii kuboresha biashara zao na kuongeza mapato ya serikali kupitia sekta ya utalii wilayani Siha”, amesema.
Aidha amesema kuwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Shamba la Misitu West Kilimanjaro, imekuwa mmoja wa wadhamini wa tamasha hilo ikiwa ni kuitikia agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lililowataka (TFS) kuwa wabunifu ili kukuza, kuongeza ajira na kukuza kipato kupitia taasisi hiyo.
“Maelekezo ya Rais kwa TFS, alitutaka kuacha kutegemea aina moja ya chanzo cha mapato na ndipo tukaja na wazo la kuandaa tamasha hili kila mwaka”, alisema na kuongeza, mbali na kuhamasisha utalii, pia tamasha hilo linalenga kuhamasisha uhifadhi wa Mazingira, jambo ambalo tumekuwa tukihamasisha shughuli za utalii ili kusudi mazingira yetu yaendelee kuwa salama”.
Ameongeza kuwa “Idadi ya washiriki wa tamasha hili imekuwa ikongezeka kila mwaka; mwaka huu yamefanyika ndani ya msitu wa asili tofauti na miaka mitatu ya nyuma ambayo mashindano yalikuwa yakifanyika nje ya msitu, hili litasaidia kuwavutia watu pale watakapoona uoto wa asili na hivyo kuhamasika kuyatunza mazingira”, alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa West Tour Kili Marathon Mensieur Elly amesema tamasha hilo limewahusisha zaidi ya washiriki 500 ikilinganishwa na washiriki zaidi ya 400 waliokuweko mwaka jana.
“Tamasha hili linaendelea kukua kila mwaka; washiriki wote wa mwaka huu, wamefurahia kupita katika maeneo ya asili ya uhifadhi , yaliyotulivu na kujionea nanma msitu ulivyotunzwa vizuri kupitia na TFS”, amesema.
Amesema mbali na mandhari nzuri pia washiriki wameweza kuona wanyama pori wakiwemo Tembo, Nyati, Twiga, Ndege aina mbalimbali, Maporomoko ya maji pamoja na mabwawa ya asili.
“Tamasha hili lilihusihsa mbio za Km 5, Km 10 na mbio za 21 kupitia kwenye msitu mnene, kuendesha baiskeli kwa umbali wa Km 10 pamoja na mbio za pikipiki kwa umbali wa km 21.
Pia amesema kuwa mbio za mwaka 2024, ambazo huandaliwa na TFS kupitia Shamba za Misitu la West Kilimanjaro lililoko Wilayani Siha, zimehusisha washiriki kutoka New Zealand, Uholanzi, Ujerumani, Marekani, Afrika Kusini, Ufaransa, Congo, Kenya, Uganda, India na wenyeji Tanzania.