Taasisi ya Uchapishaji wa vitabu ya Africa Proper Education Network (APE-Network) imeanza mikakati itakayowezesha uanzishwaji wa maktaba ya kisasa wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kujenga utamaduni wa wananchi kujisomea kila wanapopata nafasi.
Mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo Hermes Salla, ameyasema hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Amkeni Tujenge Mkomongo (ATM) iliyofanyika kijiji cha Mkomongo Kata ya Kibosho Magharibi, Wilayani humo.
Amesema kuwa wanafunzi wengi haswa wale walioko shule za msingi hukosa vitabu kwa ajili ya kujisomea jambo ambalo alisema linapunguza ari ya watu kupenda kusoma vitabu hata kwa wale ambao wana nia ya kufanya hivyo.
“Ili kukabiliana na hali hiyo, tumeanza mkakati wa kujenga maktaba nzuri na ya kisasa ambayo itakuwa na vitabu vya kutosha kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kujisomea”, amesema Salla.
Aidha amesema katika kutimiza azma hiyo, kampuni yake itawezesha ukarabati wa chumba kimoja katika shule ya msingi Mkomongo ambacho kitatumika kama maktaba, kazi ambayo alisema inatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi 1.3 milioni.
Katika hafla hiyo, kampuni imechangia vitabu 210 vyenye thamani ya Sh milioni 2.5 kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne na la saba katika shule ya msingi Mkomongo.
“Huu ni mwanzo wa mpango wetu mkubwa unaolenga kuhakikisha wanafunzi wakuwa katika mazingira mazuri ya kujisomea; lengo kuu ni kuhakikisha tunakuwa na maktaba kubwa kwa ajili ya wanafunzi na wananchi wengine”, amesema.
Ameongeza, “Ili kufanya zoezi la uendeshaji wa maktaba hii, kutakuweko na zoezi la kuchangia gharama, ambapo wqnafunzi, wazazi na wananchi wengine watakuwa na fursa za kujiandikisha kama wanachama jambo ambalo litawesha maktaba hiyo kuwa na vitabu vingi na hivyo kuwa endelevu”.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa Chama cha ATM, Salla amewapongeza waanzilishi wake ambapo alisema kitakuwa ni chachu ya maendeleo ya eneo hilo na wananchi wake kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekeiti wa Chama cha ATM Daniel Mboya, amesema kuwa chama hicho kina malengo sita ambayo alisema ni pamoja na kukuza elimu, Uchumi, mazingira, afya, usalama wa wananchi na michezo.
“Swala la elimu tumelipa kipaumbele kikubwa kutokana na ukweli kuwa elimu ndiyo itakuwa ni taa ya kumulika na kutekeleza hayo malengo mengine”, amesema Mwl. Mboya.
Pia ameipongeza Kampuni ya APE Network kwa mchango wake wa vitabu ambapo alisema vitabu hivyo vitakuwa ni msingi katika kukuza elimu kupitia chama kilichoanzihswa cha ATM.
Ameendelea kusema kuwa Desemba, mwaka huu, chama hicho kinatarajia kuandaa tamasha kubwa ambalo litawakutanisha wana Diaspora wote wanaotoka eneo la Mkomongo ili kukaa pamoja na kuweka malengo yatakayowezesha kuleta mabadiliko Chanya ndani ya eneo hilo.
Naye mkuu wa shule ya Msingi Mkomongo Frederick Kitali, ameishukuru Kampuni ya APE-Network kwa mchango wa vitabu hivyo ambapo alisema mchango huo umekuja wakati muafaka haswa ikitiliwa maanani ya kuwa ukosefu wa vitabu vya kujisomea ni changamoto kubwa haswa kwa shule za msingi.